Arsenal waiondoa Leicester City kwenye Carabao Cup
Na MASHIRIKA
MABAO kutoka kwa beki Christian Fuchs aliyejifunga na mvamizi Eddie Nketiah yaliwapa Arsenal ushindi wa 2-0 dhidi ya Leicester City katika mechi ya Carabao Cup uwanjani King Power mnamo Septemba 23, 2020.
Ufanisi huo wa Arsenal sasa umewakatia tiketi ya kuvaana na Liverpool au Lincoln katika raundi ya nne ya kivumbi hicho mwezi ujao.
Liverpool watakuwa wageni wa Lincoln leo Septemba 24 katika mchuano wa raundi ya tatu.
Fuchs alijifunga katika dakika ya 57 baada ya kugongwa na mpira ulioelekezwa langoni na fowadi Nicolas Pepe.
Nketiah alizamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kushirikiana vilivyo na beki Hector Bellerin.
Awali, kiungo James Maddison wa Leicester alishuhudia kombora lake langoni pa Arsenal likigonga mhimili wa goli. Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa raia huyo wa Uingereza kuchezea Leicester muhula huu wa 2020-21.
Ushindi wa Arsenal dhidi ya Leicester uliendeleza rekodi nzuri ya kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta ambaye aliwaongoza vijana wake kuwapiga Liverpool kwenye Community Shield msimu huu kabla ya kupepeta Fulham na West Ham United kwenye mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Ingawa Arteta alikifanyia kikosi chake mabadiliko saba, Arsenal walisalia thabiti na imara katika idara zote licha ya kukosa huduma za viungo Mesut Ozil na Matteo Guendouzi kwa mara nyingine.
Bukayo Saka alidhihirisha ukubwa wa ushawishi wake uwanjani kwa mara nyingine huku Nketiah akiwa tishio kwa mabeki wa Leicester mara kwa mara.
Ozil hajachezeshwa na Arsenal katika mchuano wowote tangu kurejelewa kwa msimu wa 2019-20 mnamo Juni 2020. Kabla ya kusitishwa kwa soka ya Uingereza kwa sababu ya corona mnamo Machi 2020, Ozil alikuwa tegemeo kubwa la kocha Arteta katika mechi zote za Arsenal kuanzia Disemba 2019.