• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Mafuriko yalivyotatiza wakulima Perkerra

Mafuriko yalivyotatiza wakulima Perkerra

Na KEVIN ROTICH

KIWANGO kikubwa cha maji katika ziwa Baringo kimeathiri mradi wa unyunyiziaji mashamba maji wa Perkerra, ulioko Kaunti ya Baringo, baada ya maji ya ziwa hilo kuvunja kingo na kufurika hadi ulipo mradi huo.

Kwa sasa, mradi wenyewe umefunikwa na maji hayo na katika mashamba ya karibu mimea kama mahindi, nyanya, vitungu na mboga imetapakaa kote, baada ya kung’olewa na kuachwa juu ya ardhi.

Ni mradi ambao umekuwa ukiwafaa wakazi wa eneo hilo kwa zaidi ya miongo mitano sasa, ukisaidia ukuzaji mimea katika shamba lenye ukubwa wa ekari 3, 000, hali iliyowapa wakazi pato la kila siku.

Lakini, mradi huu sasa unatishiwa na maji yanayozidi kuongezeka katika maziwa ya Baringo na Bogoria, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha eneo la Marigat kipindi cha Julai na Agosti.

Katika ziwa Baringo, kwa mfano, kiwango cha maji kiliongezaka kwa asilimia 60 na katika ziwa Bogoria yakapanda hadi kilomita 44.

Wakazi wanaoishi maeneo hayo wamelalamika kupata hasara kubwa kufuatia hali hiyo, wakisema itaathiri kiwango cha chakula wanachotarajia kuvuna msimu huu.

Mmoja wa wakulima walioathirika ni Kevin Lekoseki ambaye alisema kuwa shamba lake la ukubwa wa ekari tatu lilifunikwa na maji.

Kwa sasa, Bw Lekoseki analazimika kutumia boti anapozuru shamba lake, kutokana na kiwango kikubwa cha maji.

“Maisha yamekuwa magumu kwani shamba ninalotegemea limeharibiwa. Kwa sasa, siwezi panda mimea yoyote kwani mchanga umeloa maji,” Bw Lekoseki akasema.

Alisema hali hiyo imemfanya kushindwa kukidhi mahitaji ya familia yake kwani hakuna kazi, na ameishia kupoteza ajira iliyokuwa ikimpa hadi Sh50, 000 kwa wakati mzuri kila mwaka, katika upanzi wa mahindi.

Lakini anashukuru kuwa hakupoteza mifugo yake 53 ambayo alifanikiwa kuiokoa, japo akihofia kuwa maji yakiendelea kuongezeka huenda akawapoteza wanyama hao.

“Kuanzia janga ili lianze, nilihama kutoka sehemu nilipokuwa nikiishi na nimekuwa nikihama hama zaidi ya mara tatu kutafuta mahali salama,” akasema. Sasa mkulima huyo anaiomba serikali kuwahamishia katika mahali palipo juu na salama.

Kilomita chache kutoka kwake ni nyumbani kwa Issa Lesambur ambaye naye shamba lake la ukubwa wa ekari mbili limeharibiwa.

Kila anapoliangalia, kumbukumbu za miezi kadhaa iliyopita wakati shamba hilo lilikuwa limejaa mimea zinamjia, akikosa kuamini kuwa sasa halina chochote.

Kwa kawaida, Bw Lesambur hupanda mahindi, maharagwe, mboga na ndengu lakini msimu huu hajapanda chochote. Atapoteza Sh100, 000 mwaka huu, anasema.

“Mafuriko haya yamefanya Maisha yangu kuwa magumu kwani shamba hili ndilo tegemeo langu la pekee,” anasema.

Mradi wa Perkerrra ulianzishwa kwa mara ya kwanza mnamo 1956, kabla ya Kenya kupata uhuru. Japo ulikuwa na changamoto za kuwa na wakulima wachache walioutumia, mnamo 1996, wakulima walianza kupanda mahindi kwa wingi baada ya kushirikiana na Shirika la Kenya Seed (KSC) na upanzi wa mahindi uliponoga, wakulima wakaasi upanzi wa Papaya, Chili, Kitunguu, Pamb na Tikiti Maji.

Kilichofuata ni kuenea kwa mradi wa kunyunyuzia maji katika maeneo ya Mosuro, Kamoskoi, Eldume, Sandai na Kapkuikui. Vyanzo vya maji vinavyotegemewa ni vya Molo, Waseges, Kiserian na Lorwai.

Kulingana na Bodi ya Unyunyiziaji Maji nchini (NIB), mradi wa Pekerra ni tegemeo kwa familia 13, 000 eneo hilo, kando na maelfu ya watu wengine katika kaunti za Baringo na Nakuru.

Mnamo 2018, kwa mfano, wakulima walipanda mahindi katika ekari 2,200 baada ya kupokea mbegu kutoka kwa mashirika ya KSC na Monsanto.

Kaunti ndogo ya Marigat, Baringo ambapo mradi huo unapatikana, hupokea mapato ya Sh54 million kila mwaka kutoka kwa mavuno.

Bi Esleen Tarkok anasema kuwa tangu alipofika eneo la Perkerra zaidi ya miaka 60 iliyopita kutoka eneo la Kasoiyo, Kabarnet, hajawahi kushuhudia kuongezeka kwa maji kiwango hicho.

“Nimewasomesha watoto wangu saba kutoka kwa mradi wa Perkerra na sijawahi kuona janga kama hili,” Bi Tarkok akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wavumbua mashine inayoua virusi vya corona kwenye vifaa

Kazi ya uandishi mitandaoni inalipa