Makala

WINNIE MACHARIA: Nina mpango wa kuwasaidia waigizaji chipukizi

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

”KAMWE umri hauwezi kuzima ndoto ya uigizaji wengi hushiriki mpaka kipindi wanaondoka duniani.” Haya ni matamshi yake, Winnie Wangui Macharia mwenye umri unaozidi miaka 40 anayefunguka kwamba ndio ameanza kucheza ngoma wala hana nia ya kung’atuka katika ulingo wa burudani ya maigizo.

Msanii huyu aliyeanza kujituma kwenye masuala ya uigizaji mwaka 2015 anatoa mwito kwa wapenzi wa filamu wakae ange kumtazama kwenye runinga ya Citizen TV akishiriki katika kipindi kinaovuma sio haba hapa nchini cha Maria anakofahamika kama Patricia.

”Ingawa nimeanza kushiriki filamu miaka michache iliyopita tayari nimegundua nina talanta ya uigizaji,” alisema na kuongeza kwamba ndani ya kipindi hicho amefahamu kwamba uigizaji ni ajira kama nyingine.

Mwigizaji huyu ambaye kwenye kipindi cha Uriro wa Wendo (mafumbo ya upendo) anajulikana kama Mrs Munene anasema alianza uigizaji kama mzaha tu baada ya kupigwa kalamu alikokuwa anafanya kazi katika makao ya watoto mayatima ya SOS.

”Nakumbuka vizuri binfasi sikuwa najihusisha na masuala ya filamu lakini baada ya kupoteza ajira dadangu Grace Irungu alinishauri nijaribu uigizaji katika kipindi cha pendo Series ambapo nilishiriki majaribio na kupata nafasi kama Nesi. Mwandishi wa filamu huyo alivutiwa na uigizaji wangu na kunipa nafasi kukuza talanta yangu. Hivyo ndivyo nilianza uigizaji wangu ambapo kufikia muda huu kamwe siwezi kujutia lolote.”

Msanii huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa pia matangazo ya kibiashara na kampuni tofauti ndani ya miaka mitano iliyopita ambayo amekuwa katika tasnia ya uigizaji. Ameshiriki kipindi hicho cha Uriro wa Wendo ambacho hupeperushwa kupitia runinga ya Inooro TV pia ‘Mzia Mazi’ ambayo hupeperushwa kupitia Maisha Magic East.

Mwanamaigizo huyu anasema amepania kuanzisha brandi yake na kusaidia waigizaji chipukizi ambao wamefurika katika maeneo tofauti kote nchini.

Katika mpango mzima anasema miaka mitano ijayo itakuwa mshauri wa waigizaji wanaibukia pia analenga kuwa mwandishi wa filamu za Kikuyu.

”Ili kupaisha kiwango cha filamu zetu hapa nchini maprodusa na wamiliki wa mashirika ya televisheni wanahitaji kupanga uigizaji katika kiwangio cha ajira hasa kwa kuwalipa wahusika vizuri,” akasema na kuongeza kwamba malipo duni huvunja waigizaji wengi moyo na kusepa.

Ingawa baadhi ya Wakenya wanapenda kutazama filamu za kigeni mwigizaji huyu anasema wanamaigizo wa humu nchini wanafanya kazi nzuri ambapo anatoa mwito kwa wafuasi wao wazidi kuwapa sapoti kwa kutazama kazi za wazalendo.

Anashauri wasichana wanaokuja kwamba wanastahili kufanya utafiti zaidi kuhusu masuala ya uigizaji endapo wanapania kupiga hatua kwa kazi zao pia wasijishushe hadhi huku wakifahamu chochote wanaume ambacho hufanya pia mwanamke anaweza kufanya.

Kadhalika anawaambia wasichana wanaojihisi wanacho kipawa wajiunge na vikundi ya uigizaji ili kukuza talanta zao. Anashukuru babake mzazi PG Macharia, familia yake bila kuweka katika kaburi la sahau wafuasi wake.