• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Sharp Boys wapangia wapinzani vichapo

Sharp Boys wapangia wapinzani vichapo

NA JOHN KIMWERE

TIMU ya Sharp Boys kwa wasiozidi umri wa miaka 14 bado inaamini ina uwezo tosha kuvuruga mahasimu wao wa tangu jadi Kinyago United.

Sharp Boys ambayo hutiwa makali na kocha, Boniface Kyalo ni kati ya vikosi vimevyoendelea kunoa talanta za wachezaji chipukizi katika mitaa ya Majengo, Kinyago, Kitui Village katika eneo bunge la Kamukunji. Sharp Boys chini ya nahodha, Wyne Orata ilifanya kweli na kumaliza nafasi ya pili kwenye mashindano ya ‘Covid is the Enemy’ Uwanjani Kinyago wiki mbili zilizopita.

Sharp Boys iliibuka ya pili ilipochapwa mabao 3-2 na Kinyago United katika fainali kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka sare bao 1-1.

Kwenye nusu fainali, Sharp Boys ilijikatia tiketi ya fainali ilipozamisha Pro Soccer Academy kwa mabao 4-2 baada ya kutoshana nguvu mabao 2-2.

”Bila kujisifia ninaamini chipukizi wangu wamekaa vizuri kufanya kweli kwenye michezo ya Ligi ya KYSD ambayo huandaliwa kila mwaka. Kuibuka nafasi ya pili kwenye kipute cha juzi ni dhihirisha tosha tuna uwezo wa kubeba ubingwa wa ligi,” Kyalo alisema na kuongeza kuwa wanatarajia kujituma kwa udi na uvumba kwenye kampeni za muhula ujao.

Kocha huyo anadokeza kikosi chake ni miongoni mwa timu bora eneo hilo ambapo anatamani sana kuona vijana wake wakibeba taji hilo linaloshikiliwa na Kinyago United. ”Kinyago United imeshinda taji hilo kwa zaidi ya mara 20 ambapo ni vizuri timu nyingine nayo ibebe kombe hilo na ndio maana ninatamani kutawazwa mabingwa wa kipute hicho,” akasema.

Kocha huyo anasema msimu uliyopita walikuwa wamepania kubeba kombe hilo lakini matumaini yao yaligonga ukuta walipomaliza nafasi ya nne kwenye jedwali.

”Sharp Boys hutumia soka kuwaleta pamoja vijana chipukizi ili kuwasadia kupiga chenga matendo maovu mitaani ikiwamo matumizi ya mihadarati kati ya mengine. Juhudi zetu zimesaidia wengi kupiga hatua kimasomo ambapo vijana tisa wanasoma vyuo vikuu mbali mbali nchini pia wenzao 20 ni wasomi wa shule za upili tofauti nchini.”

Pia kocha huyo anajivunia kuwa Melvin Kamau ambaye ameajiriwa kama askari wa magereza aliyepitia mikononi mwake. Sharp Boys imenoa makucha ya wachezaji wengi tu ambao huchezea vikosi tofauti ambavyo hushiriki mechi za Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Orodha yao inashirikisha: Tryon Omondi (Posta Rangers Youth), Bravin Omondi (Tusker Youth), Christopher Muriithi (Nunguni FC ya Machakos), Hussein Maina, William Okwasumi na Sudeis Hussein wote Uprising FC. Uprising iliyokuwa inashiriki mechi za Nairobi East Regional League (NERL) tayari imefuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

  • Tags

You can share this post!

WINNIE MACHARIA: Nina mpango wa kuwasaidia waigizaji...

Wakenya watatu wapinga kuvunjwa kwa Bunge