Olunga sasa apata ukame wa mabao
Na GEOFFREY ANENE
MICHAEL Olunga anaonekana kukaukiwa na mabao tena baada ya kukamilisha mechi mbili bila bao katika ushindi wa Kashiwa Reysol wa 1-0 dhidi ya Hokkaido Consadole Sapporo kwenye Ligi Kuu ya Japan, Jumatano.
Mshambuliaji huyo Mkenya hakuona lango dhidi ya Sanfrecce Hiroshima mnamo Septemba 19 timu yake ya Kashiwa ikikabwa 1-1 uwanjani Hitachi Kashiwa.
Katika mechi ya hivi punde iliyochezewa uwanjani Sapporo Dome mbele ya mashabiki 3002, Olunga alipoteza nafasi tatu kabla ya kocha Nelsinho kumpumzisha dakika ya 84 na kuingiza Hiroto Goya katika nafasi yake.
Ni mechi ya kwanza katika orodha ya tisa zilizopita ambayo Olunga hajachezeshwa dakika zote 90. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya mwenye umri wa miaka 26 pia alikuwa amepoteza nafasi kadha dhidi ya Hiroshima. Kiungo Hidekazu Otani alifungia Kashiwa bao lililozamisha Sapporo dakika ya 52.
Katika michuano mingine iliyosakatwa Jumatano, FC Tokyo ilizaba Cerezo Osaka 2-0, Gamba Osaka ikapepeta Nagoya Grampus 2-1 nayo Kashima Antlers ikalemea Shonan 1-0. Kawasaki Frontale imeadhibu Yokohama 3-2, Vissel Kobe ikachapa Sagan Tosu 4-3 nayo Oita Trinita ikakubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Hiroshima. Urawa Red Diamonds imevuna alama tatu muhimu dhidi ya Shimizu katika ushindi wa 2-1 nao mabingwa watetezi Yokohama Marinos wakaliza Vegalta Sendai 3-1.
Baada ya mechi za raundi hiyo ya 18, Kawasaki imefungua mwanya wa alama 11 juu ya jedwali kwa kuzoa alama 50. Inafuatiwa na Cerezo (39), Tokyo (38), Kashima (33) nayo Kashiwa inafunga mduara wa tano-bora kwa alama 30 sako kwa bako na Nagoya, Marinos na Urawa zinazoshikilia nafasi za sita, saba na nane, mtawalia.
Olunga, ambaye pia alikosa kufunga bao katika mechi tatu baada ya ligi kurejelewa Julai 4, anasalia juu ya orodha ya wafungaji akiwa ametikisa nyavu mara 16 kwenye ligi hii ya klabu 18.
Anafuatiwa na Wabrazil Everaldo (Kashima) na Marcos Junior (Marinos) ambao wamefunga magoli 11 kila mmoja.
Mechi ijayo ya Kashiwa ni dhidi ya Marinos mnamo Septemba 27.