Kazuyoshi Miura avunja rekodi ya uzee ligini Japan
NA MASHIRIKA
KAWASAKI:
Ligi Kuu ya Soka ya Japan (J1 League) anayonogesha Mkenya Michael Olunga, ilishuhudia rekodi ya mchezaji mzee kuwahi kuishiriki ikivunjwa na mshambuliaji Kazuyoshi Miura kuchezea klabu yake ya Yokohama FC hapo Septemba 23, 2020.
Miura, ambaye alianza kutandaza soka ya malipo mwaka 1986, alikuwa katika kikosi cha Yokohama kilichopoteza 3-2 dhidi ya Kawasaki Frontale uwanjani Todoroki.
Alishiriki mechi hiyo akiwa na umri wa miaka 53, miezi sita na siku 28. Miura alifuta rekodi ya Masashi Nakayama aliyevalia jezi ya Consadole Sapporo akiwa na umri wa miaka 45, miezi miwili na siku moja mwaka 2012.
Kazu, anavyofahamika Miura kwa jina la utani, aliwahi kuibuka mchezaji bora wa ligi hiyo mwaka 1993 akiwa mchezaji wa timu ya Verdy.
Kabla ya kuweka rekodi mpya hapo Jumatano, Kazu, ambaye aliwahi kuwa nyota katika timu ya taifa ya Japan, alikuwa amechezea Yokohama mechi mbili mwezi uliopita, lakini kwenye Kombe la Levain Cup.
Hapo Jumatano, Kazu alitwikwa majukumu ya nahodha katika mechi ambayo alijituma vilivyo kabla ya kumpumzishwa dakika ya 56 na nafasi yake kujazwa na mshambuliaji chipukizi Koki Saito, 19.
Hii ilikuwa mechi ya kwanza kabisa ya Kazu kwenye Ligi Kuu ya Japan katika kipindi cha miaka 13. Kazu pia anashikilia rekodi ya dunia ya mchezaji mzee duniani.
Kikosi cha Yokohama kilichokung’utwa na Kawasaki pia kilikuwa na wachezaji wakongwe Shunsuke Nakamura, 42, na Daisuke Matsui,39.
– Imetafsiriwa na Geoffrey Anene