STEPHANIE MASEKI: Atumia tajriba ya uigizaji na filamu kuhamasisha umma kuhusu afya ya akili
Na DIANA MUTHEU
IWEJE leo mtu aliye na vitu vyote anavyohitaji hapa duniani kuamua kujitoa uhai?
Tutaelezaje kisa cha mtoto wa umri wa miaka minane kujitoa uhai?
Haya ni baadhi ya maswali mengi ambayo Stephanie Maseki anajaribu kuyatafutia majibu, anapojitahidi kuhamasisha jamii kuhusu Afya ya Akili.
Stephanie ni mwigizaji kutoka Mombasa, na mnamo 2017 alijitosa katika uhamasishaji jamii kuhusu maswala ya Afya ya Akili, kupitia mazungumzo ya moja kwa moja, gumzo mitandaoni na hata filamu zinazotengenezwa na kampuni yake maarufu kama Sekiba Empire.
“Mwaka huo, nilikuwa nimeshuhudia kampuni kadhaa zikipoteza wafanyikazi wengi waliojitoa uhai baada ya kukumbwa na msongo wa mawazo (depression). Jambo hili lilinisukuma kuanza kuhamasisha watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, katika mikutano na sehemu nyingine kuhusu umuhimu wa kutafuta ushauri wanapokabiliwa na maradhi hayo,” akasema Stephanie.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), msongo wa mawazo ni hali inayowakabili watu wengi duniani ambapo zaidi ya watu milioni 264 wameathirika.
Filamu ya Stephanie ya kwanza kwa jina ‘Behind the Closed Hearts’ ambayo aliizindua mwaka wa 2019 katika mtandao wa Facebook, ilikuwa inagusia mada kuhusu msongo wa mawazo, na anasema ilipokelewa vyema na umma kwa kuwa kufikia sasa, watu zaidi ya 21,000 wameitazama na kutoa maoni yao kuihusu.
“Nilipata jumbe nyingi kutoka kwa watu tofauti tofauti wakichangia mada hiyo, na pia wengine walinitia moyo niendelee na hamasa hio,” akasema.
Mnamo Jumamosi, Stephanie alizindua filamu yake ya pili kwa jina ‘Toxicity’, ambayo inazungumzia kuhusu Afya ya Akili.
Kulingana na filamu hiyo mwigizaji huyo anaonyesha vile watu wengi hung’ang’ana kutafuta maoni kutoka kwa wanajamii kama wanachofanya ni kulingana na mila na desturi ya jamii, na pale wanaposhindwa kufikia azimio lao, basi huwa wanasongwa na mawazo na hata kuwa na mafikra ya kujitoa uhai.
Kupitia filamu hiyo ambayo watu waliweza kuitazama katika ukumbi wa maigizo wa Little Theatre Club, Mombasa mnamo Jumamosi kwa mara ya kwanza, Stephanie amewataka Wakenya waache uwoga na wawe tayari kuzungumza kuhusu magonjwa ya kiakili kama vile msongo wa mawazo, na pia wasione haya kutafuta ushauri wanapopatwa na maradhi hayo.
Filamu hiyo pia itawekwa katika mitandao ya kijamii baadaye.
Stephanie alidai kuwa Wakenya na Waafrika kwa ujumla huwa na dhana kuwa swala la Afya ya Akili na magonjwa yanayohusika na hali hiyo linawaathiri wazungu pekee.
“Nimegundua Wakenya wengi hawapendi kuzungumza kuhusu mambo kadhaa, na wana mtindo wa kukaa kimya kuhusu mada kadhaa muhimu. Tumekaa kimya kuhusu Afya ya Akili, jambo ambalo limepelekea kuweko kwa visa vingi vya watu kuathirika vikali na hata idadi ya vifo vya watu ambao wameathirika na hali hiyo kuongezeka. Mbona hatuzungumzii maswala haya? Tumenyamaza sana kuhusu maswala muhimu hadi msongo wa mawazo unawauwa watu wengi,” akasema Stephanie.
Alitoa wito kwa Wakenya kuanza mazungumzo ya wazi kuhusu Afya ya Akili haswa wakati huu mgumu uliosababishwa na janga la Corona, ambapo watu wengi wameripotiwa kufanya mambo yasiyo ya kawaida kama vile wanawake kuwaua waume zao kwani hawakuwa wamezoea kukaa pamoja kwa muda mrefu, na wengine kujito uhai kwa kuwa walipoteza kazi zao.
“Mazungumzo hayo ni muhimu sana kwa kila mtu, watoto kwa wazazi, wazee kwa vijana, mabibi kwa mabwana na mameneja kwa wafanyikazi,” akasema Stephanie.
Alitoa wito kwa mashirika ya serikali na binafsi kuunga mkono mazungumzo kuhusu Afya ya Akili, ili kuhakikisha ujumbe unamfikia kila mtu, kwa kuwa limekuwa swala nyeti katika jamii ya sasa.
Meneja wa Bodi ya kutathmini Ubora wa Filamu Nchini (KFCB) eneo la Pwani, Bw Boniface Kioko aligusia kwamba maradhi ya Covid-19 yameathiri sana ajira kwa vijana, lakini kupitia filamu kama hizo ambazo zimeandikwa na kuigizwa na vijana, na ambazo zinaelimisha, zinaburudisha, zinafunza kuhusu mada muhimu ikiwa ni pamoja na Afya ya Akili, mizozo nyumbani na dhuluma za kijinsia; kuna mwanga kuwa mambo huenda yakabadilika na kuwa mazuri.
Bw Kioko Aliahidi kuhakikisha kuwa usambazaji wa ujumbe katika mada yaliyogusiwa unafanywa kwa kufuata miongozo iliyowekwa kuzuia kuenea kwa Covid-19.
Alibaini kuwa sanaa inaweza kueneza ujumbe kuhusu Afya ya Akili kwa njia rahisi na wazi.
“KFCB itashirikiana na vijana hawa kuendesha ajenda ya kupitisha ujumbe huo kwa umati, kwa nia ya kubadilisha mawazo ya umma kuhusu maswala kadhaa muhimu,” alisema Bw Kioko.
Alisema idara hiyo imewasaidia vijana kuwa na jukwaa ambalo wanaweza kulitumia kuonyesha kazi zao mbalimbali za kuleta maendeleo, na pia kuwasaidia kupata vifaa muhimu kama vile ukumbi wa maigizo wa Little Theatre Club ambapo huwa wanaonyesha filamu zao na kuigiza.
Bw Kioko alisisitiza kuwa tasnia ya ubunifu ni mojawapo ya biashara yenye faida tele pale ambapo wahusika wataichukulia kwa uzito, na aliwahimiza vijana kuwa mstari wa mbele kutengeneza filamu safi.