Kocha Bilic wa West Brom apigwa faini ya Sh1.1 bilioni kwa kumchemkia refa wakati wa mechi
Na MASHIRIKA
KOCHA Slaven Bilic wa West Bromwich Albion amesisitiza kwamba “sijafanya kosa lolote” licha ya kukubali kutozwa faini ya Sh1.1 milioni kutoka kwa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA).
Mkufunzi huyo raia wa Croatia alionyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza katika mechi iliyokutanisha kikosi chake na Everton kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 20, 2020.
Chini ya kocha Carlo Ancelotti, Everton walisajili ushindi wa 5-2 katika mechi hiyo iliyochezewa uwanjani Goodison Park.
“Nilizungumza na vinara wa FA na wasimamizi wa klabu ya West Brom baada ya mechi hiyo. Licha ya kuwasisitizia kwamba hakuna kosa nililokuwa nimefanya, bado nilipokezwa faini,” akatanguliza.
“Ingawa sikubaliani kabisa na maamuzi hayo, nimekubali faini kwa sababu ndiyo njia rahisi zaidi ya kuondokea balaa, Kusahau yaliyojiri na kumakinikia vibarua vilivyopo mbele yetu,” akasema kocha huyo.
Bilic, 52, alichemka ugani Goodison na kuanza kuzomea refa Mike Dean aliyemwadhibu beki wa zamani wa Arsenal, Kieran Gibbs kwa kumkabili vibaya fowadi mpya wa Everton, James Rodriguez aliyeagana na Real Madrid mwanzoni mwa mwezi huu.
West Brom watakuwa wenyeji wa Chelsea uwanjani The Hawthorns mnamo Septemba 27, 2020, na Bilic ambaye hakupigwa marufuku, ataruhusiwa kukaa katika sehemu ya makocha baada ya kutozwa faini.