Kai Havertz afunga mabao matatu na kusaidia Chelsea kuponda Barnsley 6-0 kwenye Carabao Cup
Na MASHIRIKA
MABAO matatu kutoka kwa sajili mpya Kai Havertz yalisaidia Chelsea kuwapepeta Barnsley 6-0 katika mchuano wa Carabao Cup mnamo Septemba 23, 2020.
Mabao hayo yalikuwa ya kwanza Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 21 kufungia Chelsea tangu asajiliwe kutoka Bayer Leverkusen mwanzoni mwa mwezi huu kwa kima cha Sh9.9 bilioni.
Tammy Abraham aliwafungulia Chelsea ukurasa wa mabao katika dakika ya 19 na akachangia mabao yote matatu yaliyofumwa wavuni na Havertz kunako dakika za 28, 55 na 65 mtawalia.
Magoli mengine ya Chelsea yalifungwa na Ross Barkley na Olivier Giroud katika dakika za 49 na 83 mtawalia.
“Nafurahishwa na Kai. Aliridhisha kila alipopata mpira na hii ni mojawapo ya mechi ambazo nadhani zitampa msukumo wa kujituma hata zaidi katika vibarua vijavyo. Hapana shaka kwamba atajiamini sasa na kufunga idadi kubwa ya mabao,” akasema kocha Frank Lampard.
Mabao matatu ya Havertz yalikuwa ya kwanza katika kikosi cha watu wazima kwenye taaluma ya soka. Hadi kufikia sasa, amehusika katika mabao 26 kwenye mashindano yote ya mwaka wa 2020 ambapo amefunga 18 na kuchangia mengine manane.
Ni Robert Lewandowski (35), Lionel Messi (32) na Cristiano Ronaldo (31) pekee ambao wamehusika katika ufungaji wa mabao mengine zaidi hadi sasa mwaka huu wa 2020.
Chelsea kwa sasa watakutana na mshindi kati ya Tottenham na Leyton Orient katika raundi ya nne ya kipute cha Carabao Cup.
Mechi kati ya Tottenham na Leyton Orient iliyokuwa isakatwe mnamo Septemba 22 iliahirishwa baada ya idadi kubwa ya wanasoka wa Leyton kuugua ugonjwa wa Covid-19.
Havertz alikuwa kati ya wanasoka watatu waliounga kikosi cha Chelsea kilichopokezwa kichapo cha 2-0 na Liverpool katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 20, 2020 uwanjani Stamford Bridge.
Mechi kati ya Chelsea na Barnsley ilimpa Lampard jukwaa mwafaka la kumwajibisha beki Thiago Silva, 36, kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe kutoka Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa mwanzoni mwa Septemba.