Spurs wapewa tiketi ya bwerere baada ya wanasoka 17 wa wapinzani wao kwenye Carabao Cup kuugua Covid-19
Na MASHIRIKA
TOTTENHAM Hotspur wamepatiwa tiketi ya moja kwa moja kushiriki hatua ya 16-bora ya Carabao Cup baada ya mchuano wa raundi ya tatu uliokuwa uwakutanishe na Leyton Orient kufutiliwa mbali.
Hatua hiyo ilichangiwa na tukio la idadi kubwa ya wanasoka wa Orient (wachezaji 17) kuuguza ugonjwa wa Covid-19 na kutiwa kwenye karantini.
Vinara wa Soka ya Uingereza (EFL) walishauri Orient kukatiza ndoto ya kuwania ubingwa wa Carabao Cup baada ya kuthibitisha kwamba hawangeweza kupambana na Spurs kwa mujibu wa kanuni za shindano hilo.
Mchuano uliokuwa uwakutanishe Orient na Walsall katika Ligi ya Daraja la Tatu nchini Uingereza (League Two) pia umeahirishwa.
Spurs kwa sasa watavaana na Chelsea kwenye hatua ya 16-bora ya Carabao Cup mnamo Septemba 29, 2020, uwanjani Tottenham Hotspur Stadium.
Mechi hiyo itatandazwa siku tatu baada ya Spurs kuvaana na Newcastle United na siku tatu kabla ya kukutana na Maccabi Haifa FC ya Israel kwenye Europa League mnamo Oktoba 1, 2020.