COVID-19: Bado hakuna kupumua
Na WANDERI KAMAU
WAKENYA wataendelea kukabiliwa na ugumu wa kiuchumi kwa miezi sita ijayo, hata ikiwa Rais Uhuru Kenyatta atafungua uchumi hapo Jumanne wiki ijayo, imeonyesha ripoti mpya.
Rais anatarajiwa kulihutubia taifa Jumanne kueleza ikiwa Serikali itaendelea kutekeleza baadhi ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona au la.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Ijumaa na Shirikisho la Waajiri Kenya (FKE), mashirika mengi yameathiriwa vibaya na janga hilo kiasi kwamba huenda yakashindwa kuwalipa wafanyakazi wake kwa miezi sita ijayo.
Mashirika hayo sasa yanaitaka Serikali kubuni hazina maalum ambayo itayasaidia kushughulikia baadhi ya mahitaji ya kimsingi ya wafanyakazi hao.
“Kupitia hazina hiyo, waajiri wanatarajia kupata usaidizi wa kifedha utakaowawezesha kusuluhisha baadhi ya changamoto zinazowakabili,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa FKE, Bi Jacqueline Mugo.
Asilimia 51 ya mashirika hayo yalisema yatalazimika kupunguza matumizi ya fedha kushughulikia masuala ya kimsingi ya wafanyakazi wao ikiwa hayatapata namna ya kujiokoa.
“Tunaiomba Benki Kuu ya Kenya (CBK) kushirikiana na benki zingine kubuni mkakati utakaotusaidia kulipa mikopo bila kutuumiza,” ikaeleza FKE kwenye ripoti.
Kama njia ya kuyawezesha kujisimamia tena kiuchumi, makampuni hayo yanaitaka Serikali kuondoa marufuku ya usafirishaji bidhaa nyakati za usiku ili kuwawezesha Wakenya kuboresha mapato yao tena.
Mashirika mengi yamekuwa yakiripoti kupata hasara huku mengine yakilazimika kupunguza idadi ya wafanyakazi wao kutokana na kushuka kwa mapato.
Mnamo Mei, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kutoa Sh53.7 bilioni kuzisaidia sekta nane zilizoathiriwa zaidi na janga hilo. Miongoni mwa sekta zilizolengwa ni utalii, vijana, wenye biashara ndogondogo kati ya sekta zingine.
Licha ya juhudi hizo, Wakenya wengi wamekuwa wakilalamikia kutofaidika kwa mikakati hiyo.
Hilo linajiri huku ikibainika kuwa jumla ya Wakenya 1.7 milioni walipoteza ajira zao kati ya mwezi Machi na Juni kutokana na hatua ya serikali kufunga shughuli za kiuchumi.
Halmashauri ya Kitaifa ya Kukusanya Takwimu (KNBS) ilisema kuwa kwa jumla, nafasi za ajira zilishuka kutoka 17.6 milioni hadi 15.9 milioni.
Halmashauri hiyo ilisema kuwa vijana walio chini ya umri wa miaka 35 ndio walioathiriwa zaidi.
Hali hii imetajwa kuwa pigo kubwa kwa maelfu ya vijana wanaomaliza masomo yao katika vyuo mbalimbali kila mwaka.
Asilimia 20 ya waajiri walisema mikakati hiyo haijawasaidia kujiinua kiuchumi hata kidogo, huku asilimia 60 wakiikosoa kwa kutochukua juhudi za kutosha kuwaokoa dhidi ya athari za corona.
Ripoti hiyo vilevile ilisema kuwa mapato katika mashirika hayo yalipungua kwa zaidi ya asilimia 84 kwenye kipindi hicho, huku mifumo wa usambazaji bidhaa ikishuka kwa asilimia 66.
Wafanyabiashara ndogodogo nao wamekuwa wakilalamika kutofikiwa na fedha zilizotengwa na serikali kuwawezesha kuzichukua kama mikopo ya kufufua biashara zao.
Baadhi ya mikakati kama ‘Kazi Mtaani’ pia imekosolewa na baadhi ya wataalamu wa kiuchumi, wakisema mipango ya kuwasaidia vijana inapaswa kuwa ya muda mrefu.
Serikali imekuwa ikishinikizwa na wadau mbalimbali, hasa wenye vituo vya burudani na kuuzia vileo kuwaruhusu kurejelea biashara zao kutokana na kupungua mwa maambukizi ya virusi hivyo.
Hata hivyo, Rais Kenyatta amekuwa akishikilia kuwa atafungua uchumi tu kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa wataalamu.