• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
Obado atakavyombwaga Raila katika kukuru kakara za Migori

Obado atakavyombwaga Raila katika kukuru kakara za Migori

Na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa weledi na ukakamavu wa Gavana Zachary Okoth Obado, kisiasa ndio kizingiti kikuu dhidi ya juhudi za ODM kumtimua afisini kwa tuhuma za ufisadi.

Wadadisi wanasema kutokana na sifa hizi na mtindo wake wa uongozi usiobagua wakazi wa Migori kwa misingi ya kikabila au tabaka, zimemfanya kupendwa na raia licha ya masaibu tele yanamzonga mahakamani na ndani ya ODM.

Hii ndiyo maana madiwani 41 wangali wamegawanyika kuhusu msukumo wa chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga kwamba Obado atimuliwe baada ya mahakama kuamuru asiingie afisini hadi kesi inayomkabili itakapoamuliwa.

Gavana Obado alishtakiwa mnamo Agosti 31, pamoja na wanawe wanne, kwa tuhuma za kupora jumla ya Sh300 milioni, pesa za umma katika serikali ya Kaunti ya Migori.

Waliachiliwa huru kwa dhamana ya Sh8.7 milioni, pesa taslimu, lakini Hakimu Lawrence Mugambi akaamuru kwamba aSItie guu katika afisi yake hadi kesi itakapokamilika.

Siku mbili baada ya uamuzi huo kutolewa, ODM iliandaa mkutano wa madiwani wa chama hicho, jijini Nairobi na kupanga hoja ya kumtimua Obado. Lakini ni madiwani 38 kati ya 41 waliohudhuria mkutano huo huku duru zikisema baadhi yao walipinga mpango wa kung’olewa afisini kwa gavana huyo.

Kufikia wiki hii, madiwani wa bunge la Kaunti ya Migori hawajafaulu kujadili suala hilo licha ya kufanya vikao vinane tangu walipoagizwa na uongozi wa chama kufanikisha hoja ya kumwondoa afisini Bw Obado. Hii ni licha ya ODM kupitia mwenyekiti John Mbadi na Katibu Mkuu Edwin Sifuna kutishia kuwaadhibu madiwani watakaopinga kutimuliwa kwa gavana huyo.

Ukaidi wa madiwani washirika wa Bw Obado ulidhihirika Jumatano pale walipovamia kikao cha bunge la Kaunti ya Migori kilichokuwa kikiendeshwa na Naibu Spika George Omamba, kujadili suala la kutimuliwa kwa gavana huyo.

Diwani maalum Mary Ogodo alivunjika mkono wakati wa purukushani hizo na akalazwa hospitalini.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa za Luo-Nyanza, Bw Odoyo Owidi anasema itakuwa vigumu kwa ODM kufaulu katika juhudi zake za kumng’oa Gavana Obado afisini kwa sababu gavana huyo amefaulu kagawanya madiwani wa chama hicho.

“Ukweli ni kuwa Obado anafahamu kitambo kwamba uongozi wa ODM haujawahi kumsamehe kwa kushinda chaguo lao katika chaguzi za 2013 na 2017. Hii ndiyo maana aliamua kupalilia uhusiano mzuri na wananchi pamoja na madiwani. Si siri kwamba baadhi ya madiwani wa ODM na Jubilee hupewa kandarasi katika serikali ya Migori kutokana na usaidizi kutoka kwa Gavana Obado,” anasema, akiongeza kuwa mkakati huo umemwezesha Obado kudhibiti bunge la Kaunti ya Migori.

Katika uchaguzi wa 2013, Bw Obado alimshinda aliyekuwa mgombeaji wa ODM, Prof Edward Oyugi licha ya kuwa aliwania kiti hicho kwa tiketi ya chama kisicho na ufuasi mkubwa Migori, People Democratic Party (PDP). Hii ni baada ya Obado kupokonywa ushindi katika mchujo wa ODM.

Baada ya kurejea ODM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Obado alimbwaga Ochilo Ayacko (sasa Seneta wa Migori) katika mchujo wa chama hicho uliokumbwa na fujo si haba.

Hii ni baada ya wafuasi wa gavana huyo kulalamikia kile walichotaja kama njama ya ODM kumpokonya ushindi.

Bw Owidi anaongeza kuwa Gavana Obado amefaulu kupata umaarufu miongoni mwa raia kutokana na hulka yake ya kushirikiana na makundi ya kijamii kupitia kundi la Sengwenya ambalo husawiriwa kama “jeshi la Obado”.

“Mtandao ambao Bw Obado ameujenga mashinani kwa kufanya kazi na makundi ya akina mama na vijana katika wadi zote za Migori umeimarisha ukuraba kati yake na wananchi wa kawaida. Hii ndiyo maana wananchi wengi wamekuwa wakimtetea licha za kesi za mauaji na ufisadi zinazomwandama korti,” akasema.

Mnamo 2018 gavana huyo alishtakiwa baada ya kuhusishwa na kifo cha aliyekuwa mpenziwe, Sharon Otieno, aliyekuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Rongo.

Majuzi Obado alishikilia kuwa atafanya kila awezalo kusambaratisha mipango ya ODM ya kumtimua afisini akiitaja kama inayoongozwa na chuki. Akizungumza katika kituo cha redio kinachopeperusha matangazo kwa lugha ya Dholuo mnamo Jumatano jioni, gavana huyo anayetumikia muhula wake wa pili, alikiri kuwa uhusiano wake na ODM haujawa mzuri tangu 2013.

“Mbali na kunitimua kutoka wadhifa wa ugavana, ninasikia wanapanga kuniondoa kutoka orodha ya wanachama wa ODM kwa kisingizio kuwa ninakabiliwa na kesi ya ufisadi! Mbona hatua kama hiyo haijachukuliwa dhidi ya mwenzangu Sospeter Ojaamong, ambaye pia akabiliwa na kesi ya ufisadi? Na mbona wakati ule walikuwa wapesi kumtetea Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru dhidi ya kutimuliwa kwa makosa haya haya?” Bw Obado akauliza.

Lakini ODM inashikilia kuwa ilipendekeza Obado aondolewe mamlakani kwa lengo la kuzuia kukwama kwa shughuli za utoaji huduma katika Kaunti ya Migori baada ya mahakama kumzuia gavana huyo kuingia afisini.

Bw Mbadi, ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini anasema endapo Naibu Gavana Nelson Mahanga atahudumu kama kaimu gavana, hali hiyo haitaimarisha shughuli za utoaji huduma kwa sababu hatakuwa na mamlaka ya kufanya mabadiliko yoyote katika serikali hiyo.

“Kama kaimu gavana, Mheshimiwa Mahanga hawezi kuwafuta kazi, kuwahamisha au kuwateua mawaziri na maafisa wengine wakuu katika serikali ya Kaunti ya Migori kwani, kulingana na Katiba, gavana pekee ndiye anayeweza kutekeleza mabadiliko kama hayo. Hii ndiyo maana chama cha Jubilee kiliunga mkono kubanduliwa kwa aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu baada ya mahakama kumzuia kuingia afisini, ilivyomzuia Obado,” anaeleza Bw Mbadi.

Bw Mbadi anaongeza kuwa naibu huyo wa Gavana wa Migori hajawa akitekeleza majukumu yoyote na ndiyo maana hajawa na uhusiano wa karibu na mawaziri wa kaunti hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna anashikilia kuwa msimamo wa chama hicho kuhusu ufisadi ni kwamba “endapo pana ushahidi, tutahimiza wahusika waadhibiwe kwa mujibu wa sheria”.

Bw Owidi anasema licha ya ODM kujipiga kifua, itakuwa kazi ngumu kwake kumtimua Gavana Obado kutoka wadhifa huo.

“Hii itaonekana kama pigo la kisiasa kwa Bw Odinga ikizingatiwa kuwa Bw Obado anasawiriwa kuwa mwandani wa Naibu Rais William Ruto,” anaongeza.

You can share this post!

Maswali 10 ya ‘Tangatanga’

Yachukua miaka 49 Southampton kuangusha Burnley katika EPL