Man-United kumtuma kiungo Andreas Pereira hadi Lazio kwa mkopo
Na MASHIRIKA
MANCHESTER United wamekubaliwa na Lazio kuhusu mpango wa kumwachilia kiungo wao matata Andreas Pereira ajiunge na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Italia kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Pereira, 24, amekuwa mchezaji wa Man-United tangu 2014. Hata hivyo, amewahi kuwajibikia Granada FC na Valencia za Uhispania kwa mkopo katika kipindi hicho.
Tangu 2014, Pereira alikosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Man-United hadi msimu uliopita wa 2019-20 ambapo aliwajibishwa mara 40 katika mashindano yote.
Hata hivyo, alipangwa katika kikosi cha kwanza mara moja pekee na kutokea benchi mara sita tangu ujio wa Bruno Fernandes wa Ureno aliyechezeshwa na Man-United kwa mara ya kwanza mnamo Februari 1 dhidi ya Wolves.
Kuja kwa Bruno uwanjani Old Trafford kulimweka Pereira katika ulazima wa kusugua benchi kambini mwa Man-United kiasi kwamba hajawajibishwa katika mechi yoyote kati ya tatu zilizopita ambazo kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kimetandaza.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO