Kipchoge kutumia kiatu kilichomtambisha Ineos 1:59 katika London Marathon
Na CHRIS ADUNGO
ELIUD Kipchoge atatumia viatu aina ya ‘Nike Alpha fly N%’ wakati wa mbio za London Marathon, Uingereza mnamo Oktoba 4.
“Viatu vina rangi ya bendera ya Kenya kuwakilisha watu wema wa nchi hii,” akaandika Kipchoge kwenye mtandao wake wa Facebook.
Kipchoge atakuwa pia akiadhimisha mwaka mmoja tangu aweke historia ya kuwa binadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya muda wa saa mbili alipotawala Ineos Challenge kwa saa 1:59:40.2 mwaka jana. ‘Alpha fly N%’ ndicho kiatu ambacho Kipchoge alivalia wakati wa mbio hizo zilizoandaliwa jijini Vienna, Austria.
Mbali na rangi za bendera ya Kenya, kiatu hicho pia kina herufi ‘EK’ zinazoashiria ufupisho wa jina ‘Eliud Kipchoge’ na ‘1:59:40’ ambao ni muda ulioandikishwa na bingwa huyo wa dunia jijini Vienna.
Kivumbi cha London kitatoa jukwaa kwa Kipchoge kutoana jasho na Mwethiopia Kenenisa Bekele ambaye ni binadamu wa pili duniani mwenye kasi zaidi katika mbio za marathon.
Bekele nusura avunje rekodi ya dunia ya saa 2:01:39 iliyowekwa na Kipchoge katika marathon jijini Berlin, Ujerumani mnamo 2018 alipokamilisha mbio za Berlin Marathon kwa saa 2:01:41 mwaka jana.
Kiatu cha Kipchoge kiliibua hisia mseto baada ya mbio za Ineos 1:59 Challenge huku baadhi ya wakosoaji wakitaka kipigwe marufuku kutokana na wepesi wake.
Hata hivyo, Kipchoge na kampuni ya Nike walisisitiza kwamba ufanisi katika mbio hautegemei kiatu bali mtazamo wa anayekivalia.
“Viatu hivyo havijapigwa marufuku licha ya kuzungumziwa sana. Natazamia kuvitumia tena nitakapolenga kutetea ufalme na kutwaa taji la tano la London Marathon,” akasema Kipchoge aliyeibuka mshindi wa mbio hizo mnamo 2015, 2016, 2018 na 2019.
Bingwa mtetezi wa London Marathon kwa upande wa wanawake, Brigid Kosgei pia alitumia viatu vya ‘Alpha fly N%’ alipoweka rekodi mpya ya dunia katika marathon. Kosgei alikamilisha Chicago Marathon kwa saa 2:14:04, siku moja baada ya Kipchoge kuwika jijini Vienna mnamo Oktoba 12, 2019.
Viatu hivyo vya sampuli ya ‘Vaporfly’ kutoka Nike, vimetengenezwa kwa teknolojia inayomwezesha mtumiaji kuchapua miguu kwa kasi ya juu ajabu.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), kila kiatu kipya kitakachotengezwa baada ya Aprili 30 mwaka huu, kitahitajika kuwa sokoni kwa zaidi ya miezi minne kabla ya mwanariadha kuwa huru kukitumia. IAAF imeagiza kupigwa marufuku kwa viatu vyote vilivyo na soli za ndani zenye ukubwa wa zaidi ya milimita 40.
Mbali na Kipchoge, kikosi cha Kenya kwa upande wa wanaume kinajumuisha bingwa wa Amsterdam Marathon, Vincent Kipchumba na bingwa wa Rotterdam Marathon, Marius Kipserem. Wengine ni Benson Kipruto na Gideon Kipketer aliyeibuka bingwa wa Mumbai Marathon mnamo 2016.
Kwa upande wa wanawake, bendera ya Kenya itapeperushwa na Edith Chelimo, Kosgei, Vivian Cheruiyot aliyeibuka mshindi wa London Marathon mnamo 2018, bingwa wa dunia Ruth Chepng’etich na mshindi wa Frankfurt Marathon, Valary Jemeli.
“Mbio za London Marathon ni kibarua kikubwa. Ingawa hivyo, nimejiandaa vya kutosha na natazamia kubwaga wapinzani na kuvuna matokeo ya kuridhisha,” akasema Chepng’etich ambaye hujifanyia mazoezi katika eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado.
Mwaka jana, Kipchoge alitawala mbio za London Marathon kwa muda wa saa 2:02:37 mbele ya Waethiopia Mosinet Geremew (2:02:55) Mule Wasihun 2:03:16 walioambulia nafasi za pili na tatu mtawalia.
Kwa upande wa wanawake, Kosgei aliibuka mshindi kwa muda wa saa 2:18:20 na kumpiku Cheruiyot aliyeridhika na nafasi ya pili (2:20:14). Roza Dereje aliambulia nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:20:51.
“Kivumbi cha London Marathon kitakuwa na upekee na msisimko mkubwa. Kitashirikisha wanariadha wa haiba ya juu na kibarua nilicho nacho si chepesi,” akatanguliza Kipchoge.
“Niko katika hali nzuri na fomu yangu inaridhisha. Kubwa katika matamanio yangu ni kutetea taji. Lakini hali ya hewa ikisalia shwari jinsi ilivyo, nitawazia uwezekano wa kuvunja rekodi yangu,” akaongeza.