Dimbi la majitaka linavyohatarisha maisha ya wakazi wa Nairobi
Na SAMMY WAWERU
Utupaji wa taka na suala la majitaka jiji la Nairobi na viunga vyake ni kati ya changamoto ambazo zimekuwa zikitatiza jiji hilo ambalo ni sura ya Kenya kwa wageni wanaotua nchini kutoka mataifa ya kigeni.
Ni tatizo ambalo linaendelea kuzua hatari ya mazingira, hususan katika mitaa ya mabanda na pia katika baadhi ya mitaa ambayo inaendelea kuimarika.
Katika mojawapo ya kikao na wanahabari Afya House, wakati akitoa taarifa ya maambukizi ya Homa ya virusi vya corona (Covid-19) nchini, Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya, Dkt Mercy Mwangangi alikiri uchafuzi wa mazingira kupitia utupaji taka kiholela “ungali changamoto kuu hasa katika Kaunti ya Nairobi.
Dkt Mwangangi alitoa kauli hiyo, kutokana na swali la wanahabari kuhusu kero la utupaji maski kiholela wakati ambapo serikali na wadau husika wanapambana kudhibiti msambao wa corona.
Katika mtaa wa Zimmerman, ulioko kiungani mwa jiji la Nairobi, taswira hiyo si tofauti, kuanzia utupaji taka kiholela, maski, hadi majitaka.
Kero la majitaka mtaani humo linaendelea kuwa dondandugu kwa wenyeji. Hata hivyo, kinachokera zaidi ni yanakoelekezwa yanapoachiliwa kutoka kwenye ploti au majengo ya makazi.
Kwa muda wa miezi kadhaa, Taifa Leo imekuwa ikiendesha uchunguzi wa mitaro ya majitaka eneo hilo. Mikusanyiko ya majitaka imeelekezwa katika mtaro unaotoka eneo la Base, pembezoni mwa Kamiti Road.
Unapokea aina zote za taka zinazoachiliwa kutoka kwa ploti na majengo ya makazi. Mkondo wake unafuata barabara inayounganisha Kamiti Road na Thika Road.
Katika umbali wa takriban mita 500, mtaro huo unapinda kushoto na mita chache mbele, unaelekea katika mojawapo ya kipande cha ardhi kinachoonekana kuwa mahame.
Majitaka hayo yanaunda dimbwi, dimbwi ambalo kulingana na wakazi kando na kuchafua mazingira, ni hatari katika usalama wao. “Hili ni dimbwi hatari la majitaka, limekuwa hapa kwa muda wa zaidi ya miaka mitano. Limezingirwa na ploti zenye wapangaji, na baadhi yetu tuna watoto,” mama mmoja aliyetambua kama Trizah akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.
Hata ingawa kimo kuenda chini cha dimbwi hilo hakifahamiki, kwa upeo wa macho linaonekana ni refu. Ni eneo ambalo kwa mujibu wa maelezo ya wenyeji hushuhudia utovu wa usalama mara kwa mara, kutokana na visa uhalifu.
“Dimbwi hili linazua hofu ya usalama, hasa jioni na usiku kwa wanaochelewa kurejea nyumbani,” anasema mkazi mwingine.
Lina mazingira yanayozua taharuki, ikizingatiwa kuwa mtandao wa magenge ya wahalifu eneo hilo pia huhangaisha watu asubuhi. “Si kisa kimoja, viwili au vitatu vya kina mama kunyang’anywa mikoba vimeripotiwa alfajiri na mapema,” anadokeza mkazi anayejitambua kama Kiragu.
Kandokando mwa dimbwi hilo, limegeuzwa kuwa dampo la taka. Kimsingi, linachafua mazingira, na endapo kuwepo kwalo hakutaangaziwa, si ajabu mkurupuko wa magonjwa kama Kipindupindu na Homa ya Matumbo ukalipuka na kuwa tishio.
Baadhi ya mifereji ya kusambaza maji Zimmerman, imepitia katika baadhi ya mitaro ya majitaka.
La kushangaza, ni eneo lenye viongozi walioko serikalini, kuanzia maafisa wa usalama kutoka kituo cha Polisi cha Zimmerman, kilichoko mita chache kutoka katika dimbwi hilo hatari, na ambao bila shaka huliona wanapopiga doria, mbunge wa Roysambu na pia diwani.
“Mwezi uliopita, Agosti 2020, Bw Waihenya Ndirangu ambaye ni mbunge wetu alizuru eneo hili kuhamasisha vijana kujiunga na mpango wa Kazi Mtaani na alipofahamishwa kuhusu dimbwi hili alituelekeza kwa MCA Peter Warutere. Umekuwa mvutano, tunarushwa kwa serikali kuu na serikali ya kaunti,” Mama Amos, ambaye ni mkazi eneo hilo kwa zaidi ya miaka mitatu anaelezea.
Ni jukumu la asasi husika za mazingira, zikiongozwa na Halmashauri ya Kitaifa ya Mazingira, Nema, kuhakikisha suala la dimbwi hilo la majitaka limeangaziwa, na ikiwezekana lizikwe kwa sababu ya hatari kimazingira na pia kiusalama linazozua.
Hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii, Nema haikuwa imetoa mwelekeo wa hatua itakazochukua baada ya kuarifiwa. “Nimepokea malalamishi na maswali kulihusu, nitawasiliana nanyi,” Meneja Mkuu wa Mawasiliano Nema, Bw Evans Nyabuto ameambia Taifa Leo.
Huku Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) ikijikakamua kuimarisha Kaunti ya Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Meja Jenerali Mohammed Badi ana kibarua, kibarua kigumu kusafisha, kung’arisha na kunadhifisha Nairobi na viunga vyake.
Meja Badi anapojibidiisha kurejesha sura ya awali Nairobi, sura ya jiji la kutamanika Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla, usafi wa mazingira hususan kutatua suala la utupaji taka kiholela na kuangazia kero la majitaka mitaani, hana budi ila kuupa kipau mbele.
Kwa wakazi wa Zimmerman, wakiwa na mahitaji mengi kuwaimarishia mtaa wao, wanaloomba litatuliwe bila kupoteza wakati ni kero la majitaka na la mno dimbwi hilo hatari la majitaka. “Lilianza kama mzaha, na sasa linaelekea kutunga usaha, linaendelea kuchafua mazingira na kuhatarisha usalama wa wenyeji.”