• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
Amonde na Injera kuongoza wanaraga watano wa Shujaa Bermuda

Amonde na Injera kuongoza wanaraga watano wa Shujaa Bermuda

Na CHRIS ADUNGO

WANARAGA watano wa timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, wameteuliwa kunogesha kipute cha dunia cha wanaraga 10 kila upande almaarufu ‘The IPL World Tens Series’ katika Kisiwa cha Bermuda mwezi huu.

Nahodha wa kikosi cha Shujaa, Andrew Amonde, ameteuliwa kwa pamoja na kigogo Collins Injera, Willy Ambaka, Oscar Ouma na Oscar Dennis kushiriki mashindano hayo.

Watano hao watakuwa sehemu ya kikosi cha SFX 10 kutoka Cape Town, Afrika Kusini chini ya ukufunzi wa mwanaraga wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Springbok Sevens’, Frankie Horne.

Nyota Cecil Afrika, 32, atakuwa miongoni mwa wanaraga watano wa ziada kutoka Afrika Kusini watakaoshirikiana na Wakenya katika kikosi cha SFX 10 – kampuni ya vyombo vya kielektroniki jijini Cape Town.

“Ni fahari tele kwamba wachezaji wa Kenya wamekubali kuwa sehemu ya kikosi chetu. Hawa ni wanaraga wa haiba kubwa wanaojivunia tajriba pevu kutokana na uzoefu wao kwenye raga ya kimataifa. Tumewateua kwa sababu Kenya ni mojawapo ya mataifa ambayo ni ngome ya wanaraga stadi barani Afrika,” akasema Horne katika taarifa yake kwa Shirikisho la Raga la Afrika Kusini (SARU) na kunukuliwa na gazeti la Daily Sun nchini Afrika Kusini.

Mechi za raundi ya kwanza ya kipute hicho Kisiwani Bermuda zitapigwa kati ya Oktoba 24-25 huku zile za raundi ya pili zikiandaliwa kati ya Oktoba 31 na Novemba 1. Michuano ya raundi ya mwisho (fainali) itasakatwa Novemba 7 uwanjani National Sports Centre, Bermuda.

Msururu wa mapambano hayo ya dunia ya wanaraga 10 kila upande yanashirikisha timu nane za wachezaji mahiri zaidi duniani wanaowakilisha watu binafsi, mashirika, asasi, taasisi au kampuni mbalimbali.

Wachezaji wote watakaoshiriki mechi hizo ndani ya viwanja vitupu wanatakiwa kufanyiwa vipimo vya corona kufikia Oktoba 15, 2020.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa Bidco United imani tele kikosi chake kitatamba...

Rhonex Kipruto atarajiwa kwenye Kip Keino Classic