• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Pigo jingine Harambee Stars baada ya Wanyama na Omollo kujiondoa

Pigo jingine Harambee Stars baada ya Wanyama na Omollo kujiondoa

Na CHRIS ADUNGO

MBALI na kukosa huduma za fowadi Michael Olunga wa Kashiwa Reysol ya Japan katika jumla ya mechi nne zijazo, timu ya taifa ya Harambee Stars imepatwa na pigo jingine.

Nahodha Victor Wanyama na kiungo Johanna Omollo hawatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Francis Kimanzi katika vibarua vijavyo vya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

“Kuna masharti makali yanayodhibiti msambao wa virusi vya corona katika mataifa wanakocheza Wanyama na Omollo. Matumaini ya kuwasadikisha waajiri wao kuwaachilia yanazidi kudidimia,” ikasema sehemu ya taarifa ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF).

Wanyama kwa sasa anachezea Montreal Impact ya Canada huku Omollo akisakatia Cercle Brugge nchini Ubelgiji.

Stars wamepangiwa kuvaana na Comoros katika mkondo wa kwanza jijini Nairobi mnamo Novemba 9 kabla ya kurudiana na kikosi hicho jijini Moroni siku nne baadaye.

Kabla ya kupigwa kwa mechi hizo za mikondo miwili dhidi ya Comoros katika Kundi G linalojumuisha pia Togo na Misri, Stars wameratibiwa kupimana nguvu na Zambia na Sudan mwezi ujao. FKF, ambayo haijathibitisha siku ya kutandazwa kwa mechi dhidi ya Sudan, imefichua kwamba gozi kati ya Stars na Chipolopolo ya Zambia itachezewa jijini Nairobi mnamo Oktoba 10.

Mnamo Jumatatu, Kimanzi alitaja kikosi cha wachezaji 34 kwa minajili ya mechi nne zijazo za Stars. Orodha hiyo ya Kimanzi imepokelewa kwa hisia mseto miongoni mwa mashabiki, akiwemo kipa wa zamani wa Gor Mahia, Mike Kisaghi.

Kisaghi amepongeza hatua ya kuitwa kambini kwa kipa Arnald Origi wa HIFK ya Ligi Kuu ya Finland na beki Clarke Oduor aliyesaidia Barnsley kukwepa shoka la kushuka daraja kwenye Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uingereza mnamo 2019-20. Chipukizi huyo alifunga bao la ushindi katika matokeo ya 2-1 yaliyovunwa na waajiri wake dhidi ya Brentford katika siku ya mwisho ya msimu mnamo Julai.

Origi atakayetimu umri wa miaka 37 mnamo Novemba 15, alivalia jezi za Stars mara ya mwisho katika mechi mbili za kufuzu kwa AFCON dhidi ya Guinea-Bissau mnamo 2016.

Ingawa hivyo, Kisaghi amekashifu maamuzi ya kuachwa nje kwa wanasoka kipa Patrick Matasi (St George SC, Ethiopia), beki David ‘Calabar’ Owino (Zesco United, Zambia), Jesse Jackson Were (Zesco), Aboud Omar (Ionikos FC, Ugiriki) na Eric ‘Marcelo’ Ouma (AIK Fotboll, Uswidi).

“Ingawa Kimanzi amejumuisha wanasoka wapya katika kikosi chake, kuna wachezaji wa haiba kubwa wanaozidi kufanya vyema kambini mwa waajiri wao ambao wametemwa kimakusudi. Hawa ni wanasoka ambao wana uwezo wa kutambisha timu ya taifa katika mechi zijazo hasa ikizingatiwa ubora wa fomu zao kwa sasa,” akasema.

Reysol wanaojivunia huduma za Olunga katika Ligi Kuu ya Japan (J1-League), wamethibitisha kwamba hawatamwachilia fowadi huyo kurejea Kenya kuwajibikia Stars kwa sasa.

Iwapo atatua humu nchini kuchezea Stars, Olunga atalazimika kukosa jumla ya michuano saba ya waajiri wake.

“Ikiwa tutamwachilia Olunga, nyota huyo huyo anayehofia pia kushuka kwa fomu yake, atalazimika kuingia karantini kwa siku 14 kabla ya kuruhusiwa tena kutuchezea. Hofu ni kwamba kwa kipindi hicho, tutakuwa na mechi muhimu ligini,” ikasema taarifa ya Reysol.

“Nilianza vyema kampeni za msimu huu wa 2020 kabla ya corona kubisha. Ligi iliporejelewa baada ya miezi minne, nilitatizika sana kufunga mabao katika mechi tatu za kwanza. Nilijinyanyua baadaye na kutikisa nyavu za wapinzani mara saba mfululizo,” akasema Olunga.

Kufikia sasa, Olunga ambaye pia amewahi kuchezea Thika United, Tusker na Gor Mahia katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL), anaongoza orodha ya wafungaji bora wa J1-League kwa mabao 17 kutokana na mechi 19 zilizopita.

Mbali na shaka kuhusu uwezekano wa kujivunia huduma za masogora wote wanaosakatia klabu za ughaibuni, Kimanzi anahofia pia namna ya kuandaa wachezaji wa ligi za humu nchini kwa minajili ya vibarua vijavyo vya Stars kutokana na ukali wa kanuni za Wizara ya Michezo na Wizara ya Afya.

FKF imesema bado inasubiri majibu ya Wizara ya Michezo kuhusu ombi la kutaka shughuli za soka zirejelewa humu nchini.

“Tumeomba Wizara ya Michezo itukubalie kuanza kujifua kwa wakati ufaao,” akatanguliza Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno.

“Gor Mahia pia wana kibarua katika soka ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) na tunahitaji pia kupata mshindi wa FKF Shield Cup ili tuwe na mwakilishi wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Conferations Cup) msimu ujao wa 2020-21,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Gor Mahia yamteua Oruro kuwa Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji

Tottenham yabadua Chelsea nje ya Carabao Cup