• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Ulinzi Stars kupigwa jeki na marejeo ya wanasoka watatu

Ulinzi Stars kupigwa jeki na marejeo ya wanasoka watatu

Na CHRIS ADUNGO

WANAJESHI wa Ulinzi Stars wamepigwa jeki na kurejea kwa wanasoka watatu tegemeo wa kikosi cha kwanza.

Kocha Benjamin Nyangweso tayari anakiandaa kikosi chake kwa minajili ya kampeni za msimu mpya wa 2020-21 na mabingwa hao mara nne wa Ligi Kuu ya Kenya wanajivunia marejeo ya mabeki Omar Mbongi na George Omondi pamoja na kiungo Kelvin Thairu.

Mbongi anarejea katika kikosi cha Ulinzi Stars baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miezi minane kutokana na shughuli za kazi tangu Januari 2020. Hatua hiyo ilimshuhudia akikosa baadhi ya mechi za mwanzo wa mwaka huu katika msimu wa 2019-20 uliotamatishwa ghafla mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Akijivunia tajriba pevu na uzoefu mpana katika Ligi Kuu ya Kenya, Mbongi pia amewahi pia kuwajibishwa na timu ya taifa ya Harambee Stars katika mechi kadhaa.

Kwa pamoja na Tusker FC ambao ni mabingwa mara 11 wa KPL, Ulinzi Stars pia walikuwa na safu imara zaidi ya ulinzi msimu uliopita ikizingatiwa kwamba walifunga idadi ndogo zaidi ya mabao.

“Ujio wa Mbongi ni afueni kubwa katika idara yetu ya nyuma. Ni beki mzoefu aliye na uwezo wa kutamba katika nafasi mbalimbali uwanjani, kuchangia mabao n ahata kufunga mengine kwa kichwa,” akasema Nyangweso.

Omondi alikuwa sehemu ya kikosi cha Ulinzi Stars katika nusu ya pili ya kampeni za msimu wa 2019-20, atakuwa akirejea kambini mwa Ulinzi Stars kwa msimu wa tatu. Sogora huyo amehitimu mafunzo ya uanajeshi katika Chuo cha RTS mjini Eldoret alikokuwa kwa kipindi cha miezi minane iliyopita.

Anarejea kambini mwa Ulinzi Stars kwa pamoja na Thairu ambaye pia amekuwa RTS. Thairu aliingia katika sajili rasmi ya Ulinzi Stars mwanzoni mwa msimu wa 2019-20 baada ya kuagana na kikosi cha Mount Kenya United. Anatazamiwa kuleta nguvu mpya na kuinua viwango vya ushindani katika kikosi cha sasa cha Nyangweso.

  • Tags

You can share this post!

Polisi waua jambazi sugu aliyejaribu kuwashambulia kwa kisu

Humphrey Kariuki aruhusiwa kusafiri ng’ambo