• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Man-City waangusha Burnley na kufuzu kwa robo-fainali za Carabao Cup

Man-City waangusha Burnley na kufuzu kwa robo-fainali za Carabao Cup

Na MASHIRIKA

MABAO mawili kutoka kwa Raheem Sterling na jingine kutoka kwa sajili mpya Ferran Torres, yalisaidia Manchester City kuwapepeta Burnley 3-0 na kufuzu kwa robo-fainali za Carabao Cup msimu huu.

Man-City walitamalaki mechi hiyo na kujivunia asilimia kubwa ya mpira huku Sterling na beki Benjamin Mendy wakimfanyia kipa Bailey Peacok-Farrell kazi ya ziada kuanzia dakika za mwanzo wa kipindi cha kwanza.

Bao la kwanza lililofuma wavuni na Sterling lilitokana na ushirikiano mkubwa kati yake na Mendy, huku la pili likichangiwa na Torres ambaye ni wing’a raia wa Uhispania aliyetokea Valencia msimu huu kwa kima cha Sh2.9 bilioni mnamo Agosti, 2020.

Mabao mawili ya Sterling katika mchuano huyo yalifikisha idadi ya magoli yake hadi 33 tangu mwanzoni mwa msimu wa 2019-20 ndani ya jezi za Man-City.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa na Leicester City kwa kichapo cha 5-2 ligini mnamo Septemba 27, 2020.

Droo ya mechi za hatua ya robo-fainali za Carabao Cup muhula huu itafanyika mwishoni mwa mechi itakayowakutanisha Liverpool na Arsenal uwanjani Anfield mnamo Oktoba 1, 2020.

Mechi dhidi ya Burnley ilikuwa ya kwanza kwa beki Aymeric Laporte kuchezea Man-City tangu augue Covid-19 mwanzoni mwa Septemba 2020. Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Man-City kukamilisha bila ya kufungwa bao tangu Julai 26, 2020.

“Hakuna asiyejua hali yetu. Kikosi kina visa vingi vya majeraha. Lakini vijana walijitahidi na kuonyesha kwamba wana kiu ya kusajili ushindi katika kila mchuano licha ya hali ya sasa,” akasema Guardiola.

Kati ya wanasoka mahiri zaidi kambini mwa Man-City ambao watasalia mkekani kwa kipindi kirefu kuuguza majeraha ni pamoja na washambuliaji Sergio Aguero na Gabriel Jesus.

Burnley kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Newcastle United ligini mnamo Oktoba 3 ugani Turf Moor huku Man-City wakiwaendea limbukeni Leeds United siku hiyo hiyo uwanjani Elland Road.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Lukaku afunga mabao mawili na kusaidia Inter kuinyuka...

Real Madrid wacharaza Valladolid na kupaa hadi kileleni mwa...