Man-United yapepeta Brighton na kutinga nane-bora Carabao Cup
Na MASHIRIKA
MANCHESTER United waliwapiga Brighton kwa mara ya pili chini ya kipindi cha siku nne mnamo Septemba 30, 2020 na kujikatia tiketi ya robo-fainali za Carabao Cup msimu huu.
Scott McTominay aliwafungulia Man-United karamu ya mabao katika dakika ya 44 kabla ya Juan Mata kufanya mambo kuwa 2-0 kunako dakika ya 73. Paul Pogba alipachika wavuni bao la tatu la Man-United kupitia frikiki kunako dakika ya 80.
Man-United walisajili ushindi huo siku nne baada ya penalti ya sekunde za mwisho iliyofungwa na Bruno Fernandes mnamo Septemba 27, 2020 kuwasaidia kuwapepeta Brighton almaarufu ‘Seagulls’ 3-2 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Ushirikiano mkubwa kati ya sajili mpya wa Man-United, Donny van de Beek na Marcus Rashford ulichangia mabao yaliyopachikwa wavuni na Mata na Pogba.
Nusura nyota wa Nigeria, Odion Ighalo awafungie Man-United bao la nne mwishoni mwa kipindi cha pili, ila fataki yake ikagonga mhimili wa goli na mpira ukatoka nje ya uwanja.
Pande zote mbili zilikamilisha mechi kwa mashambulizi makali huku kipa Jason Steele akifanya kazi ya ziada sawa na mlinda-lango Dean Henderson aliyemnyima Leandro Trossard nafasi kadhaa za wazi.
Kocha Ole Gunnar Solskjaer alikifanyia kikosi chake kilichowapepeta Brighton 3-2 awali mabadiliko 10 huku beki Victor Lindelof akiwa wa pekee aliyedumisha nafasi yake katika kikosi cha kwanza.
Brighton kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Everton katika gozi la EPL mnamo Oktoba 3 uwanjani Goodison Park huku Man-United wakiwa na kibarua kigumu dhidi ya Tottenham Hotspur ya kocha Jose Mourinho siku hiyo hiyo uwanjani Old Trafford.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO