• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Chipukizi Calvert-Lewin afunga matatu tena

Chipukizi Calvert-Lewin afunga matatu tena

Na MASHIRIKA

DOMINIC Calvert-Lewin alifunga mabao matatu katika mechi moja kwa mara ya pili msimu huu na kusaidia Everton kufuzu kwa robo-fainali za Carabao Cup mnamo Septemba 30, 2020.

Mabao matatu ya Calvert-Lewin ambaye kwa sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi kufikia sasa, yalisaidia Everton kuwaponda West Ham United 4-1 uwanjani Goodison Park.

Calvert-Lewin aliwaweka Everton kifua mbele kunako dakika ya 11 baada ya kujaza kimiani krosi ya Michael Keane.

Sogora huyo raia wa Uingereza alifunga mabao mawili mengine ya haraka katika dakika za 78 na 84 baada ya fowadi Richarlson Andrade kuwatikisa nyavu za West Ham katika dakika ya 56.

Calvert-Lewin, 23, kwa sasa anajivunia jumla ya mabao manane kapuni mwake hadi kufikia sasa muhula huu. Magoli mawili ya mwisho aliyofunga dhidi ya West Ham kwenye Carabao Cup yalichangiwa na fowadi wa zamani wa Arsenal, Alex Iwobi.

Bao la kufuta machozi ya West Ham United ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha David Moyes, lilipachikwa wavuni na Robert Snodgrass katika dakika ya 46.

Chini ya mkufunzi Carlo Ancelotti, Everton wanajivunia ufufuo mkubwa kiasi kwamba kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama tisa sawa na mabingwa watetezi Liverpool na viongozi Leicester City.

Vikosi hivyo vinavyofunga orodha ya tatu-bora kileleni mwa jedwali ndivyo vya pekee ambavyo havijapoteza mechi yoyote kati ya tatu zilizopita hadi kufikia sasa ligini msimu huu.

Everton kwa sasa wameibuka na ushindi kutokana na mechi sita zilizopita mfululizo. Iwapo watawabwaga Brighton mnamo Oktoba 3, 2020, basi wataweka rekodi ya mwanzo bora zaidi katika historia ya kikosi hicho tangu 1894.

Calvert-Lewin ameibukia vyema zaidi katika ulingo wa soka tangu aridhishe sana na kufunga bao lililowanyanyulia Uingereza Kombe la Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2017.

Moyes aliwaongoza West Ham kupepetana na Everton katika mechi hiyo ya Carabao Cup akiwa nyumbani anakojitenga tangu augue Covid-19.

Huku Everton wakijiandaa kupepetana na Brighton katika mchuano ujao wa EPL ugani Goodison Park, West Ham watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Leicester mnamo Oktoba 4 uwanjani King Power.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Macho yote kwa Kenya katika mbio za Valencia

Tottenham wamsajili fowadi Vinicius kutoka Benfica kwa mkopo