• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Uhuru kuamua kuhusu uteuzi wa Mwende Mwinzi

Uhuru kuamua kuhusu uteuzi wa Mwende Mwinzi

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi sasa anasema hatima ya Mwende Mwinzi ambaye uteuzi wake kuwa Balozi wa Kenya nchini Korea Kusini, ilikataliwa na bunge sasa uko mikononi mwa Rais Uhuru Kenyatta.

Wabunge kupitia Kamati ya Ulinzi na Masauala ya Kigeni na ile ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Bunge zilikataa uteuzi wa Bi Mwinzi kwa misingi kuwa ana uraia wa mataifa mawili; Kenya na Amerika.

Bi Mwinzi alizaliwa nchini Amerika, babake ni Mkenya na huku mamake akiwa Mwamerika.

Kwenye taarifa kwa wabunge Alhamisi alasiri Spika Muturi alisema suala hilo sasa limeondolewa bungeni baada ya mahakama mwaka jana kuamua kwamba Bi Mwende alikuwa ameasi uraia wake wa Amerika.

“Bunge hili sasa halina mamlaka katika suala hili. Uamuzi kuhusu iwapo Bi Mwende Mwinzi atateuliwa rasmi kuwa balozi wa Kenya nchini Korea Kusini sasa uko mikononi mwa Rais wa Rais hili Uhuru Kenyatta,” Muturi akasema.

Spika huyo pia alizima hoja ambayo Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji ambayo ilitaka wabunge kukataa uteuzi wa Bi Mwinzi kwa kushindwa kutimiza makataa ya Juni 6, 2019 kuasi uraia wa Amerika.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Moitalel Ole Kenta alilalamika kuwa hoja hiyo ilivurugwa bila wanachama wa kamati yake kujulishwa.

Licha ya wabunge kupinga uteuzi wa Mwende na wabunge, mwaka jana, kiongozi wa ODM Raila Odinga alitetea uteuzi huo.

Bw Odinga alisema kuwa Katiba inamruhusu Mwende kuhudumu katika wadhifa huo japo hata kama ana mataifa mawili.

Alirejelea kipengee cha 14 cha Katiba ya sasa inayosema kuwa mtu aliyezaliwa na Mkenya aliyekuwa akiishi ng’ambo, kabla ya kuzinduliwa kwa katiba hii, atachuliwa kuwa raia wa Kenya.

“Kwa hivyo, hatua ya wabunge kukataa uteuzi wa Bi Mwende kuwa balozi wa Kenya haina maana na ni sawa na kumchukulia kama mhalifu ilhali sheria na katiba inamlinda,” akasema Bw Odinga.

“Kwa kupinga uteuzi wa Mwende wabunge pia wanaua moyo na umuhimu wa uraia mbili ambayo kwayo Wakenya waliomba wapewe haki sawa ughaibuni na nyumbani ili waweze kuchangia maendeleo ya taifa letu,” akaongeza.

You can share this post!

FKF kupea timu 102 mipira

Kaunti kupokea fedha baada ya Jumanne