• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Arsenal yadengua Liverpool kwenye Carabao Cup kupitia penalti

Arsenal yadengua Liverpool kwenye Carabao Cup kupitia penalti

Na MASHIRIKA 

KOCHA Mikel Arteta anaamini kwamba kikosi chake cha Arsenal kinazidi kukua na kupiga hatua zaidi baada ya kuwapiga Liverpool 5-4 kupitia mikwaju ya penalti na kutinga robo-fainali za Carabao Cup.

Vikosi hivyo viwili viliambulia sare tasa kufikia mwisho wa dakika 90 na hivyo kulazimu mshindi kutafutwa kupitia penalti.

Kipa Bernd Leno wa Arsenal alipangua mikwaju miwili ya Liverpool kabla ya chipukizi Joe Willock kuwafungia waajiri wake penalti ya ushindi.

Wanasoka wengine waliopoteza mikwaju yao ni Harry Wilson na Divock Origi wa Liverpool; na Mohamed Elneny wa Arsenal. Penalti zilizofungwa kwa upande wa Liverpool zilichanjwa na James Milner, Georginio Wijnaldum, Takumi Minamino na Curtis Jones. Arsenal walifungiwa na Alexandre Lacazette, Cedric Soares, Ainsley Maitland-Niles, Nicolas Pepe na Willock.

Arsenal walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo ya Carabao Cup siku nne baada ya Liverpool kuwapokeza kichapo cha 3-1 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Anfield.

“Bado tuna mengi ya kujifunza, lakini tuko katika njia sawa,” akatanguliza Arteta ambaye ni mchezaji wa zamani wa Arsenal na Everton.

“Ni mara ya tatu katika kipindi cha chini ya wiki nane ambapo tumecheza dhidi ya kikosi bora zaidi katika soka ya bara Ulaya kwa sasa. Kwa mtazamo wangu, hii ni hatua nzuri katika makuzi ya kikosi kitaaluma,” akasema kocha huyo raia wa Uhispania.

“Tunataka kuchukulia kila shindano kama jukwaa maridhawa la kujishindia taji. Hilo ni jambo ambalo tutalifanya kwa bidii sana,” akaongeza Arteta.

Msimu jana, Arsenal waliambulia sare ya 5-5 na Liverpool kwenye hatua nyingine ya 16-bora katika Carabao Cup kabla ya kocha Jurgen Klopp kuongoza kikosi chake kudengua Arsenal kwa mabao 5-4 kupitia penalti.

Leno, 28, aliweka historia ya kuwa kipa wa kwanza wa Arsenal kutofungwa na Liverpool uwanjani Anfield baada ya Vito Mannone mnamo Septemba 2012.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Aston Villa katika EPL mnamo Oktoba 4, 2020 uwanjani Villa Park huku Arsenal wakiwaalika Sheffield United ugani Emirates kwa kivumbi cha EPL siku hiyo hiyo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Tineja Ansu Fati aweka historia ya ufungaji wa mabao...

Harry Kane afunga matatu na kusaidia Spurs kuponda Maccabi...