Harry Kane afunga matatu na kusaidia Spurs kuponda Maccabi Haifa 7-2
Na MASHIRIKA
NAHODHA Harry Kane alifunga mabao matatu naye Dele Alli akapachika moja katika ushindi mnono wa 7-2 uliosajiliwa na Tottenham Hotspur dhidi ya Maccabi Haifa ya Israeli kwenye mechi ya kufuzu kwa hatua ya makundi ya Europa League.
Mechi hiyo ilikuwa ya saba kwa Tottenham kusakata katika kipindi cha siku 19 tangu kufunguliwa rasmi kwa kampeni za msimu huu wa 2020-21.
Jumla ya mabao matano yalifungwa kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza huku Tottenham, waliokuwa wakichezea nyumbani, wakicheka na nyavu za wapinzani wao mara nne.
Kane alifungulia Tottenham karamu ya mabao katika dakika ya pili kabla ya Tjaronn Chery kusawazisha mambo dakika 15 baadaye.
Bao hilo la Chery liliamsha hasira za Tottenham waliorejea uongozini kupitia kwa Lucas Moura katika dakika ya 20 kabla ya Giovani lo Celso kufunga mabao kunako dakika za 36 na 39. Mabao hayo ya Celso yalichangiwa na Steven Bergwijn na Kane.
Celso ambaye ni raia wa Argentina, aliondolewa uwanjani katika kipindi cha pili na nafasi yake kutwaliwa na Alli aliyefunga penalti mwishoni mwa kipindi cha pili.
Awali, penalti mbili zilikuwa zimepatikana mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya beki wa Tottenham Matt Doherty difenda Ernest Mabouka wa Maccabi kunawa mpira ndani ya vijisanduku vyao.
Kane alifungia Tottenham penalti iliyotokana na kosa hilo la Mabouka katika dakika ya 56 huku Nikita Rukavytsya akifunga mkwaju mwingine kwa upande wa Maccabi.
Droo ya mechi za hatua ya makundi katika Europa League msimu huu, itafanyika Ijumaa ya Oktoba 2, 2020.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO