Michezo

FKF yapiga breki mchujo kati ya Vihiga United na Kisumu All Stars

October 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

MCHUJO wa michuano ya mikondo miwili iliyokuwa iwakutanishe Vihiga United na Kisumu All Stars umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Mechi hizo zililenga kubaini klabu ya ziada itakayoshuka daraja kwenye Ligi Kuu ya FKFPL msimu ujao na ile itakayopanda ngazi kutoka Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) kwa minajili ya kinyang’anyiro cha muhula mpya wa 2020-21.

Mechi ya mkondo wa kwanza ilikuwa isakatwe mnamo Oktoba 7 na marudiano kuandaliwa Oktoba 11.

Kisumu All-Stars walishikilia nafasi ya 16 kwenye jedwali la vikosi 18 vya KPL mnamo 2019-20 huku Vihiga United wakimaliza kampeni za NSL katika nafasi ya tatu nyuma ya Bidco United na Nairobi City Stars waliokwezwa daraja kunogesha Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa mujibu wa kocha Sammy Okoth, usimamizi wa kikosi chake cha Vihiga United ulipokea taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) likiwaarifu kwamba mechi hizo zimeahirishwa kutokana na masharti makali ambayo bado yamewekwa na serikali kudhibiti msambao wa Covid-19.

“Katika barua yao, FKF, ilisisitiza kwamba kiini cha kusitishwa kwa mipango ya kuandaliwa kwa mchujo huo ulitokana na ukali wa kanuni zilizopo za kudhibiti maambukizi ya corona,” akasema Okoth.

Msimu wa 2019-20 katika Ligi Kuu ya KPL ulitamatishwa ghafla na FKF mnamo Aprili 2020 kwa sababu ya corona.

Hata hivyo, Okoth amepongeza FKF kwa hatua hiyo ya kuahirisha mchujo huo kati ya Vihiga United na All Stars, akisisitiza kwamba wengi wa wanasoka wake hawakuwa tayari kwa kibarua hicho.

“Mchakato wa kujiandaa kwa ajili ya mechi hizo ulikuwa mgumu kwa sababu ya masharti yaliyopo kutoka kwa serikali. Hiyo iliwaweka wanasoka wetu katika ulazima wa kujifanyia mazoezi,” akaongeza.

“Kuahirishwa kwa mechi hizi ni afueni kubwa hasa kwa maafisa wa benchi za kiufundi ambao hawajawahi kupata majukwaa ya kuthibitisha kiwango cha ubora wa maandalizi ambayo wamekuwa wakijifanyia,” akasema Okoth.

Wakati uo huo, kikosi cha Vihiga Bullets kinachoshiriki kipute cha NSL kipo katika hatari ya kusambaratika kutokana na uchechefu wa fedha.

“Wachezaji na maafisa wa kiufundi hawajalipwa kwa miezi kadhaa sasa na kikosi hakijawahi kurejea kambini wala kufanikisha kikao kwa minajili ya kujiandaa kwa muhula mpya kwa sababu ya hali ngumu ya kifedha,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji, Collins Juma.

Juma ameonya kwamba huenda ikawa vigumu zaidi kwa klabu ya Vihiga Bullets kufikia mengi ya maazimio yake hasa ikizingatiwa kwamba tayari idadi kubwa ya wachezaji wameagana na kikosi.

Hali sawa na hiyo, ya uchechefu wa fedha, inakabili vikosi vitatu vya Western Stima, Nairobi Stima na Coast Stima waliopoteza takriban Sh70 milioni mwaka huu baada ya kampuni ya umeme ya Kenya Power iliyokuwa ikiwadhamini kusitisha ufadhili.

Wasimamizi wa klabu hizo wamekiri kwamba wanakabiliwa na changamoto za kulipa mishahara ya wachezaji na maafisa wa benchi za kiufundi kwa sasa.

Hata hivyo, wameshikilia kwamba hali itarejea kuwa sawa kambini mwao baada ya wadhamini wapya kupatikana.

“Tumeagana na idadi kubwa ya wanasoka wa haiba kubwa muhula huu. Hata hivyo, hilo halitatutikisa kwa kuwa tunalenga kusajili chipukizi wengi pindi baada ya kupata mfadhili,” akatanguliza mwenyekiti wa Western Stima, Laban Jobita.

“Kikosi kipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na mdhamini mmoja atakayetupa ufadhili wa Sh40 milioni kwa msimu,” akasema kwa kuthibitisha kwamba wameagana rasmi na robo tatu ya wachezaji wao wakiwemo Benson Omalla, Fidel Origa, Maurice Ojwang, Stephen Odhiambo, Kelvin Wesonga, Kennedy Owino, Samuel Njau, Edwin Omondi na Abdallah Wankuru.

Kinara huyo pia amefutilia mbali tetesi kwamba Western Stima, walioambulia nafasi ya saba kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu uliopita, wanalenga kubadilisha jina hadi Keroka Football Club baada ya kupata mdhamini mpya.

Huku athari za corona zikizidi kuhisika katika sekta mbalimbali za maendeleo, zipo hofu kwamba baadhi ya vikosi vinavyofadhiliwa na mashirika, asasi na taasisi za kiserikali vitavunjiliwa mbali sawa na hali iliyofanyikia klabu za Pan Paper, Kenya Pipeline, Bata Bullets, Eldoret KCC, Rivatex na Ministry of Works FC.