Masoud Juma arejea mazoezini baada ya kupona virusi vya corona
Na GEOFFREY ANENE
Mshambuliaji Masoud Juma Choka amerejelea mazoezi baada ya kukamilisha karantini ya siku 12 nchini Algeria.
Juma,24, ambaye anachezea JS Kabylie kwenye Ligi Kuu ya Algeria, alijitenga baada ya kupatikana na virusi vya corona mnamo Septemba 18.
Hata hivyo, siku nne baadaye alisema virusi hivyo havikuonekana alipopimwa tena, ingawa bado alihitajika kukamilisha karantini yake.
Sasa Kabylie imeripoti kuwa Juma, ambaye kocha Francis Kimanzi amemjumuisha katika timu ya taifa ya Harambee Stars kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Chipopolo ya Zambia hapo Oktoba 13, ameanza mazoezi.
“Wachezaji Derragi, Daibeche, Juma, Aguieb na Ben Abdi wako chini ya ratiba maalum ya mazoezi. Osama Derragi amerejea kikosini Ijumaa pamoja na Daibeche, Juma, Aguieb na Ben Abdi chini ya naibu kocha Oudai Syphax. Wachezaji hawa watalazimika kufanya mazoezi pekee yao kabla ya kujiunga na wenzao,” klabu hiyo ilitangaza Oktoba 2.
Juma aliwahi kuvalia jezi ya Stars mara tatu, ingawa mara ya mwisho alikuwa kikosini ilikuwa wakati wa Kombe la Afrika (AFCON) 2019 alipokalishwa kitini Kenya ikilemewa na Algeria 2-0 na Senegal 3-0 na kubwaga majirani Tanzania 3-2 katika mechi za makundi mjini Cairo nchini Misri.
Kenya itapimana nguvu dhidi ya Chipolopolo ikitupia jicho michuano miwili ya kufuzu kushiriki AFCON2021 dhidi ya viongozi wa Kundi G Komoro mwezi ujao wa Novemba.
Wanavisiwa wa Komoro wanaongoza Kundi G kwa alama nne baada ya kulima Togo 1-0 mjini Lome na kulazimisha sare tasa dhidi ya Misri mjini Moroni mwisho wa mwaka 2019. Kenya na Misri zinafuatana katika nafasi ya pili na tatu kwa alama mbili mtawalia.
Vijana wa Kimanzi walikaba Misri 1-1 mjini Alexandria kabla ya kukubali sare kama hiyo dhidi ya Togo uwanjani Kasarani. Togo inavuta mkia kwa alama moja.