Everton waangusha Brighton 4-2 ligini
Na MASHIRIKA
DOMINIC Calvert-Lewin alifunga bao lake la tisa msimu huu huku James Rodriguez naye akicheka na nyavu mara mbili katika ushindi wa 4-2 uliosajiliwa na Everton dhidi ya Brighton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 3, 2020.
Ushindi wa Everton uliendeleza rekodi bora wanayoijivunia hadi kufikia sasa msimu huu ambao umewashuhudia wakiibuka na ushindi katika mechi zote nne za ufunguzi wa muhula na kutua kileleni mwa jedwali kwa alama 12.
Calvert-Lewin aliwaweka Everton kifua mbele kunako dakika ya 16 kabla ya masihara ya kipa Jordan Pickford kumpa Neal Maupay fursa ya kusawazisha mambo katika dakika ya 41.
Yerry Mina ambaye ni raia wa Colombia aliwafungia Everton bao la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya kushirikiana tena na sajili mpya Rodriguez aliyepachika wavuni magoli mawili katika dakika za 52 na 70.
Brighton walifungiwa bao la pili na Yves Bissouma mwishoni mwa kipindi cha pili. Hiyo ilikuwa mechi ya tatu kwa Brighton kupoteza kutokana na nne zilizopita.
Hadi waliposhuka dimbani kuvaana na Everton, Brighton walikuwa wamecharazwa na Chelsea na Manchester United kabla ya kujinyanyua na kukizamisha chombo cha Newcastle United kwa mabao 3-0 mnamo Septemba 20, 2020.
Mbali na utepetevu wa kipa Pickford, pigo kubwa zaidi kwa kocha Carlo Ancelotti anayezidi kuongoza ufufuo mkubwa wa Everton ni jeraha alilolipata fowadi matata mzawa wa Brazil, Richarlison Andrade katika kipindi cha kwanza.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO