Coutinho avunia Barcelona alama moja dhidi ya Sevilla ligini
Na MASHIRIKA
PHILIPPE Coutinho alifuta jitihada za kiungo Luuk de Jong uwanjani Camp Nou na kuwapa Barcelona alama moja katika sare ya 1-1 dhidi ya Sevilla katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Matokeo hayo yaliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwa vikosi hivyo ligini hadi kufikia sasa msimu huu wa 2020-21.
De Jong alichuma nafuu kutokana na masihara ya mabeki wa Barcelona walioshindwa kudhibiti mpira wa kona katika dakika ya nane kabla ya Coutinho aliyerejea kutoka Bayern Munich mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 kusawazisha mambo dakika mbili baadaye.
Bao la Coutinho aliyeshirikiana vilivyo na Jordi Alba, lilikuwa lake la kwanza katika kampeni za muhula huu akivalia jezi za Barcelona.
Barcelona na Sevilla kwa sasa wanajivunia alama saba, tatu nyuma ya viongozi Real Madrid waliopepeta Levante 2-0 ugenini.
Antoine Griezmann na Lionel Messi walipoteza nafasi nyingi za kufungia Barcelona mabao zaidi katika kipindi cha pili.
Mbali na Ronald Araujo, mwanasoka mwingine aliyehangaisha zaidi mabeki wa Barcelona kwa upande wa Sevilla ambao ni mabingwa wa Europa League ni Jules Kounde ambaye alishuhudia makombora yake mawili yakigonga mhimili wa lango la wapinzani.