Habari

FUJO ZA MURANG'A: 'Tangatanga' walaumu Mutyambai

October 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

BAADHI ya wabunge wa marengo wa ‘Tangatanga’ sasa wanamlaumu Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kwa kutumiwa na “wanasiasa fulani” kuvuruga shughuli ya Kanisa, Murang’a.

Wakiongea na wanahabari Jumatatu katika majengo ya bunge, wabunge hao walimtaka Bw Mutyambai kuomba msamaha kwa viongozi wa kanisa la AIPCA, Kenol baada ya maafisa wa polisi kurusha vitoa machozi humo.

“Ni jambo la kusikitisha na kuvunja moyo kwamba Bw Mutyambai aliwaamuru maafisa wa polisi kuingia ndani ya Kanisa la AIPCA na kurusha vitoa machozi kuwatawanya waumini. Hii ni sawa na kuchafua nyumba ya Mungu,” akasema Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa.

Akaongeza: “Walipata aibu kubwa pale Mama wa Kanisa alipopiga magoti na kuomba. Nadhani huyo OCPD aliyeongoza maafisa hao waliovamia kanisa atalaaniwa.”

Naye Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua alisema mara ya mwisho ukatili kama huo kutekelezwa na polisi katika Kanisa ni mnamo Julai 7, 1997, polisi walipovamia kanisa la Anglikana la All Saints Cathedral na kuwatawanya waumini.

Wabunge wengine walioandamana nao ni; Charles Gimose (Mbunge wa Hamisi), Aaron Cheruiyot (Seneta wa Kericho), Kipchumba Murkomen (Seneta wa Elgeyo Marakwet), Purity Ngirici (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kirinyaga), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Faith Gitau (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Nyandarua) na Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali.

Wabunge hao pia waliwalaumu Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na Katibu wake Karanja Kibicho wakidai kuwa “wao ndio walitoa amri kwa Mutyambai kuwatuma polisi hao kuvuruga shughuli ya Kanisa Murang’a.”

Kulingana na wabunge, polisi waliwakinga vijana ambao walidai walisafirishwa kwa magari kutoka maeneo ya mbali kuvuruga ibada na shughuli ya harambee katika kanisa hilo.

Hata hivyo, utulivu ulirejea na harambee hiyo ikaendelea. Hata hivyo, Dkt Ruto alilaani fujo hizo na kuwasuta maafisa fulani wa serikali aliodai ndio waliwatuma polisi kuwashambulia waumini kanisani.

Jumapili jioni Inspekta Jenerali wa Polisi aliamuru kukamatwa kwa mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Kandara Alice Wahome kuhusiana na ghasia hizo.

Lakini wabunge hao wawili ambao ni wafuasi sugu wa Dkt Ruto walidai kuwa vijana waliozua vurugu siku hiyo walikodiwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Murang’a Sabina Chege.

Bi Chege alikuwa mwepesi kukana madai hayo.