Fulham wajinasia huduma za wanasoka watatu katika siku ya mwisho ya uhamisho
Na MASHIRIKA
FULHAM wamesajili Ruben Loftus-Cheek wa Chelsea na Joachim Andersen kwa mkopo kisha kujitwalia huduma za beki Tosin Adarabioyo kwa mkataba wa kudumu.
Mwingereza Loftus-Cheek na beki Andersen wa Denmark wana umri wa miaka 24 kila mmoja.
Adarabioyo, 23, amerasimisha uhamisho wake kwa mkataba wa miaka mitatu kutoka Manchester City.
“Ni furaha tele kwamba kwa sasa nitapata fursa ya kusakata soka ya EPL kwa sababu nilikosa muda kambini mwa Man-City,” akasema Adarabioyo ambaye pia amewahi kuvalia jezi za West Brom na Blackburn kwa mkopo.
Mechi yake ya mwisho kati ya nane ambazo amechezea Man-City ilikuwa Machi 2018.
Loftus-Cheek alijipata katika ulazima wa kuagana na Chelsea muhula huu baada ya kikosi hicho kufungulia mifereji ya fedha na kusajili wanasoka wanane wa haiba kubwa wakiwemo Timo Werner, Kai Harvertz, Hakim Ziyech, Xavier Mbuyamba, Malang Sarr, Ben Chilwell, Thiago Silva na Edouard Mendy.
Fulham ambao walipandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20, bado hawana alama yoyote ligini hadi kufikia sasa.
Andersen, ambaye pia amewahi kucheza FC Twente ya Uholanzi, aliagana na Sampdoria mwishoni mwa msimu wa 2018-19 na kuingia Lyon aliowachezea mechi 29 na kuwasaidia kuingia robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).