Makala

SIHA NA LISHE: Faida na manufaa ya mchaichai (lemongrass)

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WATU wengi hutumia mchaichai kama kiungo cha chai.

Faida za mchaichai kiafya

Mchaichai unaweza kutibu magonjwa kama maumivu ya tumbo, maambukizi katika njia ya mkojo (U.T.I) na pia husaidia kusafisha figo na ini.

Mmea huu pia unasaidia pakubwa kukabiliana na matatizo ya moyo, huimarisha utendaji kazi wa mishipa ya fahamu na kudhibiti mlundikano wa mafuta katika mishipa ya damu (lehemu). Vilevile, mchaichai ni muhimu katika kuondoa sumu mwilini na huongeza kinga za mwili (CD4), Huimarisha afya ya ngozi, husaidia tatizo la kukosa usingizi, hutibu maumivu ya tumbo hasa yasababishwayo na hedhi, hutoa gesi tumboni, na husaidia kukabili mafua ya mara kwa mara, hali ya kutapika na maumivu ya viungo.

Zao la mchaichai limesheheni virutubisho na misombo mbalimbali na muhimu sana kwa afya ya binadamu kama vile: Vitamin A,B1,B2,B3,B5,B6, folate na Vitamin C pamoja na madini ya potassium.

Virutubisho hivyo vinavyopatikana katika mchaichai vina uwezo mkubwa wa kuondoa mlundikano wa mafuta mwilini ambayo husababisha unene wa kupitiliza.

Pia huondoa mlundikano wa mafuta katika mishipa ya damu, hivyo kuiruhusu damu kupita vizuri katika sehemu mbalimbali za miwili.

Jinsi ya kutumia

Loweka majani ya mchaichai katika maji ya moto kiasi cha vikombe vitatu vya chai, weka majani manne kisha kunywa maji hayo kiasi cha kikombe kimoja cha chai kabla ya kula chochote asubuhi, mchana, na jioni kabla ya chajio.

Tiba ya kisukari

Virutubisho kwenye mchaichai huweka sawa kiwango cha insulini mwilini. Hivyo, kwa wagonjwa wa kisukari ambao kiwango chao cha insulini ni kidogo, wanapotumia mchaichai wanapata faida kubwa kuudhibiti ugonjwa wa kisukari.

Jinsi ya kutumia

Majani ya mchaichai huchemshwa katika maji kisha maji hayo kiasi cha kikombe kimoja cha chai yatiwe ndani unga wa tangawizi kiasi cha vijiko viwili vidogo. Kunywa maji hayo kiasi cha kikombe kimoja asubuhi kabla ya kula kitu chochote na jioni kabla ya chajio.

Hutibu vidonda vya tumbo

Chanzo kikuu cha vidonda vya tumbo ni bakteria wanaofahamika kama Helicobacter pylori. Virutubisho katika mchaichai kina uwezo mkubwa wa kuidhibiti bakteria hao hatari na hivyo kutibu ugonjwa wa vidonda vya tumbo.

Jinsi ya kutumia.

Chemsha majani za mchaichai kwa maji kiasi cha nusu lita,mgonjwa anywe maji hayo kiasi cha kikombe kimoja asubuhi na usiku kabla ya kulala.

Husafisha figo na ini

Unywaji wa chai iliotengenezwa kwa mchaichai husaidia kuondoa sumu na taka mbalimbali mwilini.

Husaidia figo na ini ambazo huhusika na kazi ya kuondoa sumu na taka katika mwili.

Hizi ni baadhi ya faida za kunywa chai yenye mchaichai:

  1. Kuzuia kutapika
  2. Kutuliza maumivu ya tumbo
  3. Kupunguza makali ya mafua
  4. Huwa na umuhimu mkubwa kwa wenye tatizo la baridi yabisi
  5. Husaidia kusafisha figo
  6. Huzuia tatizo la tumbo kunguruma
  7. Husaidia uyeyushaji wa chakula
  8. Hupunguza uwezekano wa kukumbwa na maumivu mbalimbali ya mwilini
  9. Husaidia kupunguza maumivu kwa wasichana waliobalehe na kina mama wakati wa hedhi.