Makala

Iweje mzazi wa kumzaa mtoto kabisa leo hii anamchukia?

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 6

Na MARY WANGAROI

“SIMPENDI mwanangu na nimechoka kumuumiza.” Hayo ndiyo maneno kutoka kwa mwandishi na bloga maarufu kutoka Kenya, Wanja Kavengi, ambayo yalizua gumzo mitandaoni na kuwaacha wengi vinywa wazi.

Kupitia ujumbe mrefu na wenye uzito katika akaunti yake ya Facebook, Wanja alisimulia kwa kina bila kuashiria hisia yoyote, jinsi ambavyo hajawahi kuwa na uhusiano wa karibu kama mama na mwanawe mwenye umri wa miaka minane, tangu alipokuwa amgali tumboni mwake wakati wa ujauzito hadi wakati huu ambapo alizaliwa na kutunzwa hadi kufikia umri huo.

“Sijawahi kubuni uhusiano na mwanangu. Msongo wa mawazo ulinitatiza nilipokuwa na ujauzito wake; sikumtaka. Hali hii iliendelea nilipomzaa; sikumtaka. Niligubikwa na mawazo nilipokuwa nikimkuza; sikumtaka,” akachapisha katika kijisehemu cha ujumbe wake wa kutatiza.

Akaongeza: “Nilimwona kama usumbufu, kama mzigo, kama mgeni asiyetakikana nyumbani kwangu, mwimba mchungu kwenye wayo wangu. Sikuweza kumpenda jinsi mzazi anavyompenda mtoto.”

Mwandishi huyo alisimulia jinsi alijenga ukuta wa kihisia kati yake na mtoto wake, akawa mkali kwake, akamsuta kila nafasi ilipojitokeza na kumtaja kama ‘wazo ambalo halikutarajiwa’ ‘tukio lililozuka tu kighafla.’

“Sikucheza naye, Sikucheka nayem sikula nayem sikutazama wala kusikiza chochote pamoja naye, singeenda popote naye, sikuwa na muda naye. Sikumhurumia. Nilikuwa hayawani mtesi wake aliyemwambia hapana kila wakati,”

“Sikumtaka. Singeweza kumstahimili. Sikumtimizia mahitaji yake kwa wakati ufaao na ingenichukua muda mrefu kugundua kwamba alihitaji kwenda kwa kinyozi, muda mrefu zaidi kufahamu alihitaji nguo mpya, muda mrefu zaidi kuona kuwa viatu vyake vilikuwa vimechakaa, muda mrefu zaidi kumnunulia vifaa vya kuchezea. Ningekaa sana kabla ya kumtilia maanani,” aliandika.

Uvumbuzi wa Wanja uliwaacha baadhi ya wanamitandao wakitetemeka kwa ghadhabu huku wakimkaripia vikali kwa ukatili wake dhidi ya mtoto huyo ambaye hakuwa na hatia, na aliyekuwa tu mhasiriwa wa hasira yake iliyoelekezwa pabaya.

Kulingana na mwandishi huyo, juhudi zake za kubadilisha mtazamo wake dhidi ya mwanawe, ambaye bila shaka anaathirika kisaikolojia, ziligonga mwamba na akalazimika kumwacha mwanawe mikononi mwa nyanya yake huku Wanja akijaribu kutafuta suluhisho kuhusu chochote kilichokuwa kikimhangaisha.

“Msongo wa Mawazo baada ya Kujifungua hukaa kwa muda gani? Nilifanya utafiti kwenye mitandaoni juzi kwa sababu hata nikijaribu jinsi gani, hisia zangu kwake hazijabadilika. Hali hii imedumu kwa muda mrefu zaidi. Bado sijui jinsi ya kumtunza. Mama yangu ni mama bora zaidi kwake. Kwa hakika ndiye mama bora zaidi na mama pekee ambaye amekuwa naye katika miezi michache ambayo tumekuwa tukiishi nyumbani kwa mamangu kushinda miaka yote minane ambayo nimekuwa nikiishi naye,” anasema.

Wapo waliomhurumia kuhusiana na hali kama mama aliyekuwa akililia usaidizi huku wakipongeza ujasiri wake wa kujitokeza na kuzungumza kuhusu hali yake.

Wengine wanahisi kuwa mwandishi huyo aliyebobea anatumia tu weledi wake wa kifasihi kuangazia masaibu wanayopitia kisiri kina mama na watoto. Masuala ambayo hakuna yeyote aliye na ujasiri wa kuzungumza kuyahusu.

Iwe ni uhalisia au tu sarakasi za kisanaa, jambo moja ambalo haliwezi kupuuzwa ni kuwa Msongo wa Mawazo baada ya Kujifungua (PPD) ni hali mojawapo ya afya ya akili inayopaswa kuangaziwa kwa dharura inayostahili.

Japo inastaabisha, Wanja amefichua mashaka ambayo wanawake wengi wamekuwa wakikabiliana nayo pasipo kusema lolote.

Hali huwa mbaya zaidi katika jamii za Kiafrika zinazomtarajia mama kuwa na mapenzi asilia kwa kizazi chake na ikiwa sivyo, basi atakemewa na kudhalilishwa bila huruma huku akisawiriwa kama mnyama.

Mtoto huchukuliwa kama baraka hasa katika jamii ya Kiafrika ambapo kila hatua ya binadamu inayoanza na kuzaliwa, hutiliwa maanani.

Hivyo basi, nini hasa kinachoweza kumfanya mama amchukie mtoto wake kiasi hicho baada ya kukabili miezi tisa ya kuchusha ya ujauzito?

Loise Musyoki anafahamu vyema uhalisia huu mchungu baada ya kuwa na kustahimili kipindi kigumu cha ujauzito, kujifungua na baadaye kukabiliana na PPD.

“Nilikuwa na wakati mgumu wa ujauzito na kujingua kifunguamimba wangu. Nilizirai nilipokuwa nikijifungua, walilazimika kutumia mtambo wa kuvuta mtoto kutoka tumboni. Alipoletwa kwangu, niliwaza kimoyomoyo, nilazima mngemleta sasa hivi? Lakini singetamka mawazo yangu kutokana na matarajio waliyokuwa nayo wengine,”

“Sikumkaribia kwa wiki mbili zilizofuata na ni babake aliyechukua usukani wa kumbadilisha taulo, kumwosha na kufanya kila kitu. Alipokuwa akirejea kazini nililia sana nikishindwa ni nani atakayemshughulikia. Hata hivyo, hali hiyo ilibadilika baada ya muda kutokana na usaidizi niliopata,” anaeleza.

Kwake Robin Brundage, mama wa watoto wanne, alipambana na PPD baada ya kitindamimba wake lakini kwa bahati nzuri, aliweza kuwiana vyema na mtoto wake mchanga kabla ya hali kuzorota zaidi.

“Kwa miezi sita ya kwanza ya binti yangu kitindamimba, nilihisi kana kwamba nilikuwa nikilea mtoto wa mtu mwingine, hatimaye nilimpenda lakini nahisi vibaya mno kwa kutohisi nilivyohisi na watoto wangu wa kwanza watatu,” anasema.

Kinyume na dhana kuwa PPD huduma kwa muda mfupi baada ya kujifungua na kisha kutoweka, imebainika kuwa hali hiyo inaweza kuendelea na hata kumfanya mama kumchukia mtoto wake milele jinsi Nicole Nana, mwenye umri wa miaka 35 alipogundua.

“Nina miaka 35 sasa na huwezi kunieleza kuwa mama yangu bado anaugua PPD. Kadri anavyonichukia, hatimaye nimekubali hali hiyo na imenifanya kuwa mtu anayependa sana na mama bora zaidi kwa watoto wangu kwa sababu sitaku kuwa kama mama yangu. Ninavutia nguvu kutoka kwa udhaifu,” anakiri.

Akizungumza na Taifa Leo kupitia simu, Dkt Carolyn Chakua, mtaalam wa saikolojia na masuala ya uzazi, anatahadharisha kuwa PPD inaweza kugeuka ugonjwa sugu wa kiakili endapo haitadhibitiwa kwa wakati ufaao na kuwa tishio kwa mama na mtoto husika.

“Isipodhibitiwa kwa wakati unaofaa, PPD inaweza kugeuka maradhi sugu ya kisaikolojia. Ni kama tu unapougua malaria, unahitaji matibabu ili kuzuia matatizo zaidi ya kiafya au hata kifo,” anafafanua.

Kulingana naye, kuna sababu tele zinazoweza kumfanya mwanamke kuugua PPD hadi kiwango cha kumchukia mtoto wake mwenyewe.

Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na: matukio mabaya waliyopitia utotoni, mazingira ambamo mama alitungwa mimba, kukataliwa, matatizo ya kifedha au mama hakuwa tayari kupata mtoto, PPD inaweza pia kutokana na masuala ya jeni,” anaeleza.

Mwanasaikolojia huyo ambaye pia ni mshauri wa nasaha, anaeleza kuwa kina mama wanaougua PPD hudhihirisha dalili mbalimbali huku dalili inayojitokeza zaidi ikiwa kuwakaripia watoto.

Dkt Chakua ambaye ni mwasisi wa Shirika la Kuwa Mzazi, anahoji kuwa kuwasemeza watoto kwa ukali na sauti ya juu ni dhihirisho tosha kwamba mzazi husika ana kasoro na anahitaji usaidizi.

“Kuwakaripia watoto kunamaanisha kuna kitu kinaendelea kinachomtatiza mzazi. Huwa hatuwakaripii wafanyakazi wenzetu kazini. Ikiwa unataka mtoto wako akusikize, unaweza kutumia sauti inayosikika lakini yenye utulivu. Si kupaaza sauti,”

“Kuwakaripia watoto kunaonyesha kwamba mzazi anahitaji usaidizi. Wazazi wanapaswa kuhakikisha wako wazima kisaikolojia ili kuwa wazazi bora kwa watoto wao. Kama mzazi, kuwa na uwiano na nafsi yako ya ndani ili uweze kuwa na uwiano na mtoto wako,” anasema mwanaharakati huyo wa uzazi bora.

Dkt Chakua anaamini kuwa uhusiano wa mama anayeugua PPD na mtoto wake unaweza ukanusuriwa mradi tu mtu anayeathiriwa atachukua hatua ya kwanza ya uponyaji, ambayo ni kukiri kuwa una tatizo.

“Hatuwezi kusema kuwa hali ya Wanja au mwanamke yeyote kumchukia mtoto wake ni jambo la kawaida kwa sababu kisaikolojia, kuna masuala mengi yanayochangia kilicho cha kawaida na kisicho cha kawaida. Ni ujasiri mno kwake kujitokeza na kuzungumza maadamu hatua ya kwanza ya kupona ni kukiri kuwa ana tatizo,”

“Sasa anachohitaji tu pamoja na mwanawe ni kuzingirwa na watu watakaowashika mkono na kuzungumza na watakaomwelewa na kumpa ushauri mwafaka. Anahitaji kuwasiliana na washauri nasaha na wanasaikolojia wanaoweza kumsaidia katika safari ya kupona,” anashauri Dkt Chakua.

Julius Ediwn ambaye ni wakili aliye na tajriba ya saikolojhia, anaafikiana na hisia za Dkt Chakua kuhusiana na kujijua binafsi na kutafuta ushauri wa wataalam.

“Hii ni hali fulani au ugonjwa ukipenda. Jambo nzuri ni kuwa unafahamu kuhusu hali hii na ni mwanzo mwema katika kupata suluhisho. Unahitaji mshauri nasaha au mwanasaikolojia kwa suara hilo ili kukusaidia katika safari ya kupata nafuu,” anaeleza.

Hata hivyo, anatahadharisha kuwa endapo PPD haitashughulikiwa haraka iwezekanavyo kuna hatari ya athari hizo kujirudiarudia kutoka kwa mtoto mhasiriwa na kupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi.

“Kwa bahati mbaya, ikiwa hautadhibiti hali hii kwa wakati ufaao, itaendelea kuzorota na kumwathiri mtoto na jamii katika siku za usoni. Mtoto ni mhasiriwa wa maradhi hayo lakini anaweza kunusurika ikiwa hatua itachukuliwa haraka,”

“Ingawa sayansi imethibitisha kuwa miaka ya kwanza minane ya mtoto yeyote inamfanya kuwa mtu atakayekuwa miaka ya baadaye, hiyo ni kanuni ya kijumla na kuna visa vya kipekee kwa hali hiyo. Hivyo jaribu kadri uwezavyo kutatua hali hiyo kabla wakati haujayoyoma sana,” anaeleza.

Kwa upande wake Victor Mavuti anayesomea Shahada ya Uzamifu katika Filosofia (Ph.D) katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT), masaibu ya Wanja ni kielelezo tosha cha mama aliyekwazwa anayemlea mtoto anayekwazwa hali amabyo anasema imekithiri mno katika jamii ya kisasa.

Msomi huyo anasisitiza kuwa hali hiyo ndiyo kliini cha mashaka yote katika jamii ikiwemo kusambaratika kwa mahusiano na ndoa.

Kulingana naye, wanaume wanaolelewa na kina mama waliokwazwa huishia kukwazwa, wanafunga ndoa na kuwakwaza wake zao vilevile huku msururu huo ukijirejelea.

“Mwana anayelelewa na mama aliyekwazwa, hukwazwa pia. Anamwoa binti wa mtu mwingine na kuishia kumkwaza. Msururu huo unakuwa wa kujirejelea,” anasema.

Katika siku za hivi majuzi, visa vya matatizo ya kiakili na kisaikolojia vimeongezeka pakubwa hali inayoweza kuhusishwa na uhamasishaji japo ni watu wachache wanaojitokeza kuzungumza kuhusu hali hiyo.

John Ndung’u, afisa wa uuguzi katika Huduma ya Magereza Nchini anasema kuwa masuala ya afya ya akili yanapaswa kupatiwa kipau mbele na kuwahimiza watu zaidi kujitokeza.

“Masuala ya afya ya akili yanaopaswa kupatiwa kipaumbele. Jamii inateseka na hali hiyo bila kujua la kufanya au kutofanya. Watu hawako tayari kuzungumza kuhusu tatizo hili,” anasema.

[email protected]