Ozil kugharimia mshahara wa maskoti maarufu kambini mwa Arsenal
Na MASHIRIKA
KIUNGO wa Arsenal, Mesut Ozil, amejitolea kugharimia mshahara wa Jerry Quy ambaye amekuwa maskoti aitwaye Gunnersaurus kwa kipindi kirefu uwanjani Emirates.
Mnamo Oktoba 5, 2020, Arsenal walifichua kwamba Guy, ambaye amekuwa akiwapa mashabiki na wachezaji burudani ya kipekee uwanjani kwa miaka 27 iliyopita, alikuwa sehemu ya vibarua 55 ambao watafutwa kazi baada ya hazina ya fedha ya Arsenal kulemwazwa na corona.
“Nilihuzunika sana kufahamu kwamba Jerry Quy ambaye amekuwa maskoti wetu maarufu atafutwa kazi. Amekuwa sehemu muhimu ya historia ya The Gunners,” akasema Ozil, 31.
“Kutokana na hilo, nitajitahidi kurejeshea Arsenal mshahara ambao wamekuwa wakimlipa Quy ili aendeleee kuwa sehemu ya burudani kwenye uwanjani na kwenye runinga zetu kwa sababu anaipenda sana kazi yake,” akaongeza nyota huyo mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani.
Arsenal wanaendelea na mchakato wa kufuta kazi baadhi ya vibarua 55 ili kupunguza gharama ya matumizi.
Tayari wanasoka wa kikosi cha kwanza na kocha Mikel Arteta waliafikiana na usimamizi kuhusu haja ya kupunguzwa kwa mshahara wao kwa hadi asilimia 12.5 kuanzia Aprili hadi Disemba 2020.
Vinara wakuu wa Arsenal pia walikubali kupunguziwa malipo yao kwa zaidi ya thuluthi moja kwa kipindi cha miezi 12 ijayo.
Licha ya mipango hiyo yote, Arsenal wamesisitiza kwamba wanakabiliwa na hali ngumu zaidi ya kiuchumi ambayo huenda ikadumu kwa kipindi kirefu.
Katika taarifa yao, Arsenal wamesema kwamba maamuzi ya kuwatimua baadhi ya vibarua wao hayajakuwa mepesi na yalichukuliwa baada ya kutathmini hali zote na kubaini uzito wa kifedha ambao unawakabili kutokana na janga la corona.
Idara ambazo zimeathiriwa zaidi uwanjani Emirates ni zile za uchezaji, biashara na usimamizi.
Japo miradi mingi ya maendeleo ya Arsenal kwa sasa itasimamishwa kwa muda, kikosi hicho kimesisitiza kwamba mipango yao ya uhamisho na usajili wa wachezaji haikuwa imeathiriwa na itaendelea jinsi ilivyopangwa katika muhula mfupi wa uhamisho mnamo Januari 2021.
Arsenal wamesema kwamba miongoni mwa sababu za kupungua pakubwa kwa mapato yao ni ukosefu wa mashabiki uwanjani, kufungwa kwa makavazi yao na maduka ya kuuza jezi za wanasoka wao.
Aidha, mapato kutokana na fedha za utangazaji, upeperushaji wa mechi zao moja kwa moja na ada za kiingilio zilipungua sana na kushusha shughuli zao za kibiashara tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 na shughuli za michezo kusitishwa kwa zaidi ya miezi minne kati ya Machi na Juni 2020.
Arsenal walimsajili kiungo matata raia wa Ghana, Thomas Partey kwa kima cha Sh6.3 bilioni kutoka Atletico Madrid mnamo Oktoba 5, 2020.
Ozil ambaye ni mwanasoka wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, amekuwa mchezaji wa Arsenal tangu 2013 na mkataba wake unatazamiwa kukatika rasmi mwishoni mwa muhula huu. Nyota huyo kwa sasa anapokezwa mshahara wa Sh49 milioni kwa wiki japo hajachezeshwa katika mchuano wowote hadi kufikia sasa katika msimu huu wa 2020-21.