Makala

ANA KWA ANA: Mfano halisi wa ‘ukijipata mjane usijitie unyongeni’

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na WANGU KANURI

NI matumaini ya kila mwanandoa kuzeeka pamoja na mchumba wake.

Lakini kifo kinaweza kikatokea ghafla maishani na kumteka mchumba na hivyo kuyabadilisha mambo ghafla.

Inakuwa hata vigumu zaidi ikitokea unatuhumiwa kuwa chanzo cha kifo cha mpenzi au mwenzako katika ndoa.

Vimetokea visa ambapo wajane wamenyimwa na wamewekewa vikwazo na hivyo kukosa fursa ya kuwaaga kwa heshima za mwisho wapenzi wao.

Ni wakati wa msiba ambapo utawagundua watu kwa hali zao halisi. Yote yatawekwa peupe machoni mwako. Hata ingawa mambo humuwia aliyefiwa vigumu, ujasiri wa kukubali yaliyofanyika na kuwa kielelezo kwa wengine ni ishara ya wema wa moyo.

Safu hii imekutana na Maria Muinde ambaye hata ingawa amekuwa mjane akiwa na umri wa miaka 29, anahakikisha kuwa wajane wengine wamepata pahala pa kufarijika.

Tueleze kwa kifupi, wewe ni nani?

MARIA MUINDE: Jina langu ni Maria Muinde. Mimi ni mjane, mama, mtoto, dada na rafiki. Nilikuwa nimeolewa na marehemu Tony Onyango Opondo na pamoja tukajaaliwa mtoto mmoja wa kiume ambaye anaitwa Shane Muinde Onyango.

Kifo kijapo hakibishi. Kifo ni tumbo lisiloshiba. Je wewe umewezaje kujipa moyo na kuendelea na maisha?

MARIA MUINDE: Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniongoza na kunilinda tangu siku ambayo Tony aliaga dunia. Pili nimekuwa na watu ambao wamejitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa ninaendelea vyema. Wazazi wangu walinikubali mie na mwanangu nyumbani, ndugu zangu humchukua Shane wakati ambapo nahitaji muda wangu peke yangu. Marafiki wake marehemu Tony pia hawajawachwa nyuma katika kuhakikisha kuwa tunaendelea salama.

Safari yako baada ya kufahamu kweli mpenzi wako amekuacha ilikuwa vipi?

MARIA MUINDE: Ilikuwa ngumu. Nilishtuka kisha mwili wangu ukafa ganzi. Alipotoka nyumbani siku hiyo alikuwa mwenye afya njema na alipofika nyumbani jioni hiyo ndipo aliaga usiku wa Machi, tarehe 3, mwaka wa 2020. Tony alipoaga mtu wa kwanza nilifikiria kuhusu ni mwanaetu ambaye ni mlemavu mwenye Autism ADHD. Nilishtuka ukweli wa kifo chake Tony ulipoeleweka maishani kwani ilikuwa dhahiri kuwa, licha ya kuwa mzazi wa pekee kwake Shane uzito wa kumlea peke yangu ulikuwa mikononi mwangu. Aisee Tony alikuwa kigezo kikuu.

Ni wakati wa majonzi ndipo unafahamu wanafamilia wako vyema ambapo baadhi wanaweza wakawa hawataki kusikia habari zako. Je, hisia zako ni zipi kuhusu suala hilo?

MARIA MUINDE: Kuna kujitenga kwingi mtu ajapokuwa mjane. Huwa vigumu zaidi wakati ambapo mjane huyo angali katika maisha ya ujana. Nyuma, baada ya sisi kufunga ndoa, kulikuwa na baadhi ya wanafamilia ambao walituletea kadhia nyingi na wakati ambapo Tony aliaga haswa nyumbani kwetu nilijua kuwa wanafamilia hao wangesema na kunitendea maovu. Sikukosea kwani walinitumia nyarafa za matusi huku zingine zikielekezewa wazazi wangu. Mpaka wa leo mimi hupokea vitisho vya ‘kuna utafiti upya utafanywa ili kubaini kifo chake Tony,’ lakini sibishani kwani ninachokifahamu ki wazi.

Kuna vikundi tofauti vilivyoanzishwa ili kuwasaidia kimawazo na hata kihisia wanawake waliopoteza waume wao. Je, wewe ulijihusisha na vikundi hivi?

MARIA MUINDE: Baada ya Tony kuaga, nilianza kuandika katika ukurasa wangu wa Facebook ambao ni Love Personified KE. Hii ilikuwa njia yangu ya kukubali yaliyonifika. Niliangazia kumbukumbu zangu na Tony kutoka wakati ambapo alinichumbia mpaka changamoto ambazo tulipitia katika ndoa yetu. Kuandika kwangu kuliwavutia wajane wengi na kupitia mazungumzo yangu nao, tukaanza kusaidiana na kufaana haswa katika kukubali uchungu wa yaliyotukumba. Cha kushangaza ni kwamba kila mjane aliyeniandikia ujumbe, hakuwa katika kikundi chochote kile. Wengine walikuwa wamewapoteza waume wao kitambo lakini hawakuwa katika kikundi chochote kile kwa hivyo, nikaonelea vyema kuanzisha kikundi katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp kwa jina “Tumaini na Faraja kwa Wajane.”

Uliwezaje kujiimarisha tena? Na ulichukua muda kiasi gani?

MARIA MUINDE: Sikuwa na muda wa kupumzika na kukubali yaliyotufika mimi na mwanangu kwani ujapokuwa ukipata nyarafa za ‘huyu mtoto hakuwa anatakikana’ unakubali majonzi ukiendelea na maisha. Nilikuwa na bili nafaa kulipa na nilitaka mwanangu awe na maisha mema ambayo yalitegemea nilichofanya. Kwa hivyo sikuwa na muda wa kujionea huruma bali nilianza kuhakikisha kuwa kila kitu ki sawa machoni mwa mwanangu.

Kuna njia tofauti za kueleza hisia za majonzi wakati ambapo mtu amefiwa. Wengine hujifungia nyumbani, wengine huomba, wengine hushiriki na marafiki wao, wengine hufanya kile mpenzi ama rafiki yao alifanya kabla ya kufariki. Je, wewe unaweza kuwashauri vipi watu ambao hufikiri kuwa kwa kuwa huzionyeshi hisia zako namna fulani basi kifo chake mpenzio hakikuathiri?

MARIA MUINDE: Ninaweza washauri watu kuwa katu usije ukauhukumu uchungu ambao hauelewi. Kuna mambo ama vitu ambavyo humlazimu mtu kuonyesha hisia zake haswa za kifo tofauti na kile ambacho wewe unakijua. Hata kama sikulia wala kuzoa drama haimaanishi mapenzi yangu kwa Tony yalikuwa machache.

Unaweza kuwapa moyo ama kuwashauri vipi wanawake walioachwa na wapenzio wakiwa bado wachanga haswa kwenye ndoa?

MARIA MUINDE: Biblia imesema kuwa wajane na mayatima ni wa Mungu na kile ambacho ningewarai ni kumtumainia Mwenyezi Mungu kwani atawaongoza na kuwalinda. Hamna jambo lolote ngumu kwake. Hata ingawa utasalitiwa, hakuna mtu atakayekusaidia wakati wa majonzi kumbuka kuwa watoto wako wanahitaji mzazi kwa hivyo angaza kupaa juu ya majonzi. Walinde wanako.

Ushauri wako kwa wanafamilia wa upande wa kike na wa kiume baada ya mwanandoa wa familia kumpoteza mume ama mke ni upi?

MARIA MUINDE: Wanafamilia wa pande zote mbili wanapaswa kuwa karimu kwa mjane sio kumkashifu na kuchukua mali ambayo yameachwa. Ningewasihi wawe na moyo wa huruma kwa mjane na watoto waliozaliwa katika ndoa hiyo.

Baada ya miaka kadhaa, aliyefiwa anaweza kuoa ama kuolewa. Je, hisia zako ni zipi kulingana na suala hili?

MARIA MUINDE: Mjane anaweza kuoa ama kuolewa na hii haimaanishi kuwa hakuwa anampenda mume ama mke wake aliyeaga. Muda ambao mtu huchukua kabla ya kuoa ama kuolewa unategemea na si haki kumdhihaki mjane aliyeoa ama kuolewa miaka michache baada ya kifo cha mpenzi wake. Ikiwa jamii haiwakashifu waliooana kisha wakatalikiana na mmoja wao akaoa ama kuolewa pasi kunyooshewa kidole sawa sawa mjane, akubaliwe kuoa ama kuolewa.

Ushauri wako kwa wanafamilia wa upande zote mbili haswa baada ya aliyefiwa kumpata mtu wa kumuoa ama hata yeye kuoa ni upi?

MARIA MUINDE: Iwapo amempata mtu wa kumuoa ama hata yeye mwenyewe ameoa, mnenee Baraka na umwachilie akaanze upya tena. Katika tabaka ambazo wake hurithiwa, nawasihi kama si nia yake msiendeleze mila hiyo kwake. Msisahau kuwa wajane ni watu na hata wao wangependa kupendwa na kupenda mtu na hata kuongeza idadi ya watoto.