• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
WANGARI: Wanafunzi wahitaji ushauri nasaha kukabili athari za corona

WANGARI: Wanafunzi wahitaji ushauri nasaha kukabili athari za corona

Na MARY WANGARI

MJADALA unapoendelea ikiwa shule zifunguliwe au la, itakuwa jambo la busara, mwanzo kutathmini athari za kijamii zilizowakumba watoto katika kipindi chote ambacho wamekaa nyumbani.

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, kumekuwa na matukio ya kutamausha ambapo watoto wamedhulumiwa na kutendewa ukatili na watu waliowaaminia kuwapenda, kuwatunza na kuwalinda.

Kuanzia kupigwa kinyama, kunajisiwa, kupachikwa mimba za mapema na hata kuuawa, ni baadhi tu ya masaibu ambayo yamewakumba watoto katika kipindi hiki wakiwa hawako shuleni.

Baadhi ya watoto wamelazimika kushuhudia dhuluma za kinyumbani kati ya wazazi wao baadhi zikichangiwa na hali ngumu kiuchumi.

Hali hiyo, bila shaka imeathiri pakubwa taswira waliyokuwa nayo watoto kuhusu nyumbani kama mazingira salama yaliyojawa na upendo na amani na kuwaacha na makovu yatakayochukua muda mrefu kupona.

Inasikitisha kuwa kuna baadhi ya wanafunzi ambao hawatapata fursa ya kurejelea masomo shule zitakapofunguliwa tena baada ya maisha yao kukatizwa kikatili.

Kisa cha mama aliyejitumbukiza mtoni na watoto wake wawili baada ya mgogoro wa kinyumbani, watoto wawili ambao miili yao ilipatikana ikielea mtoni baada ya kutoweka kwa muda, ni mifano tu ya uhalisia huo wa kuhuzunisha.

Si ajabu kuwa utafiti umedhihirisha kwamba kumekuwa na ongezeko la visa vya dhuluma za kinyumbani ambavyo vimesababisha familia nyingi kutengana huku watoto wakiwa waathiriwa wakuu.

Familia ni nguzo kuu kwa watoto na inaposambaratika, mtoto huathirika pakubwa kisaikolojia jambo linaloweza kuacha madhara ya kudumu.

Ili kukabiliana na matatizo hayo, baadhi ya watoto hugeukia tabia zisizo za kawaida kama vile kuwa wakaidi, kujihusisha na mihadarati au hata kushiriki ngono kiholela, yote katika jitihada za kukwepa uhalisia, kuficha uchungu na upweke walio nao.

Ni bayana kuwa walimu watakumbana na watoto tofauti kabisa na wale waliwaona awali ambapo ukaidi, kukosa kuhudhuria masomo, tabia nyinginezo za kiajabu huenda zikajitokeza. Baadhi huenda pia wameathirika kiafya.

Kwa hivyo, ni bayana kwamba walimu watahitaji neema na uvumilivu wa hali ya juu kuwapa wanafunzi muda wa kutosha kuwiana na mabadiliko hayo huku wakiwasaidia kuelewa mazingara mapya.

Ni sharti wadau husika ikiwemo walimu wabuni mikakati kabambe ya kuwezesha wanafunzi kupata mwongozo na ushauri nasaha pindi shule zifunguliwapo.

You can share this post!

MATHEKA: Uhuru atulize joto Jubilee lisielekeze nchi pabaya

TAHARIRI: Serikali italazimika kulinda wanafunzi