Makala

MWALIMU KIELELEZO: Sally Anne Karangah

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

KUWAFUNDISHA wanafunzi wa madarasa ya chini katika shule ya msingi ni kazi ngumu na pia rahisi!

Ni rahisi iwapo mwalimu – katika ufundishaji wake – atatumia mbinu zitakazompa jukwaa la kushirikiana na wanafunzi kutalii mazingira mbalimbali ya jamii inayowazunguka, kukuza viwango vya ubunifu na kuamsha ari ya kuthamini utangamano.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Sally Anne Karangah ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mwandamizi katika Shule ya Msingi ya St Lwanga inayopatikana eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa.

Akijivunia tajriba ya miaka 26 ya ualimu, Bi Sally anashikilia kwamba Mtaala wa Umilisi (CBC) umemwezesha kukuza umilisi wa wanafunzi kwa kuegemea zaidi katika upekee na ukubwa wa uwezo wao ndani na nje ya darasa.

Mbali na kujenga utaifa, uzalendo na umoja wa kitaifa, CBC inalenga kumkuza mwanafunzi ili hatimaye afikie maendeleo ya jamii kitamaduni, kiuchumi, kiteknolojia na kiviwanda. Ni mpango unaosisitiza zaidi maendeleo ya mtu binafsi ili ajitegemee katika maisha ya baadaye.

“CBC inawakuza wanafunzi kimaadili na kidini pamoja na kuwachochea kutambua umuhimu wa usawa na uwajibikaji katika jamii. Pia inawajengea wanafunzi msingi wa kuelewa mawanda mapana ya jamii ya kimataifa na umuhimu wa kuzikumbatia tamaduni za wanajamii wengine katika ujirani wao,” anasema.

Sally alizaliwa katika kijiji cha Kibugu, Kaunti ya Embu. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto wanne wa Dkt Timothy Karangah na Bi Jane Karangah aliyewahi kuwa karani katika Manispaa ya Embu. Nduguze Sally ni Dkt Edgar, Erick na Bi Christine Njiru.

Baada ya kusomea katika Shule ya Msingi ya St Michael, Embu kati ya 1976 na 1980, Sally alijiunga na Shule ya Msingi ya St Peter’s Boarding Ishiara, Embu alikofanyia mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwishoni mwa 1985.

Alifaulu vyema na kupata nafasi ya kusomea katika shule maarufu ya Kyeni Girls, Embu kati ya 1986 na 1989. Baada ya kukamilisha mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE), Sally aliajiriwa kuwa karani katika Shule ya Msingi na Shule ya Sekondari ya Kibugu.

Alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili (1990-1991) kabla ya kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St Mark’s Kigari, Embu alikosomea kati ya 1992 na 1993.

Mnamo 1994, Bi Sally aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) na akatumwa kufundisha katika Shule ya Msingi ya Mutanda, Kaunti ya Kitui. Alihudumu huko kwa mwaka mmoja kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Thiririka, eneo la Juja, Thika alikofundisha kati ya 1995 na 1996.

Bi Sally aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Msingi ya Kuraiha, Kaunti ya Kiambu kati ya 1997 na 2008. Alihamia katika Shule ya Msingi ya St Lwanga, Mombasa mwanzoni mwa 2009 na akapanda cheo kuwa Mwalimu Mwandamizi mnamo 2014.

Mbali na Bi Gladys Mugo aliyewahi kuwa Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya St Peter’s Boarding Ishiara, mwingine aliyemchochea Bi Sally kujitosa katika ulingo wa ualimu ni babu yake, Chifu Ephantus Njagi Kavungura.

“Hakuna kinachonipa fahari zaidi katika taaluma ya ualimu kuliko kutangamana na watoto wachangamfu kila tunaposoma darasani au tunaposhiriki michezo, uimbaji na utambaji wa hadithi.”

Ni raha kubwa kwa mwalimu kuona mtoto aliyeingia shuleni bila kujua lolote akipiga hatua na kuanza kufahamu kusoma na kuandika chini ya uelekezi wake,” anaeleza.

Kwa mtazamo wa Bi Sally, uzuri wa kufundisha watoto wa umri mdogo kuanzia Gredi ya Kwanza hadi Gredi ya Tatu ni kwamba wanaelewa mambo upesi, wana hamu ya kujifunza vitu vipya na wanasahau haraka hata unapowaadhibu kwa utundu wao.

“Kudumisha urafiki na watoto humfanya mwalimu kujihisi mkamilifu. Kilele cha urafiki huo ni pale wanafunzi wanapokukimbilia na kuwa radhi kukupa hadithi za kila sampuli kuhusu maisha yao binafsi,” anasema kwa kukiri kwamba ualimu ni kazi inayompa mtu jukwaa la kubadilisha maisha ya watu wengi katika jamii.

Ratiba ya Bi Sally kila siku huanza alfajiri ya saa kumi na moja na nusu. Yeye hufika shuleni mapema na mara nyingi ndiye huwa wa mwisho kuagana na lango la shule.

“Mbali na majukumu ya kawaida ya kufundisha na usimamizi wa shule, yapo mambo mengi ambayo watoto wastahili kufanyiwa. Ni wajibu wa mwalimu kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi wake na kuwa tayari kuwasaidia wanapopitia changamoto mbalimbali.”

“Msaada kwa wanafunzi wa sampuli hii ndio hunipa tija katika kazi yangu,” anaeleza Bi Sally ambaye pia ni mratibu wa programu ya Baraza la Uingereza katika Shule ya Msingi ya St Lwanga inayoshirikiana na Shule ya St Colman’s katika eneo la Annaclone, Ireland Kaskazini.

Wakfu wa Aga Khan umekuwa mstari wa mbele kupiga jeki juhudi za Bi Sally katika kuchangia maendeleo ya jamii tangu 2012. Zaidi ya mafunzo ya kumwezesha kuwapokeza wanafunzi malezi bora ya kiakademia katika eneo la Mikindani, Mombasa, Wakfu wa Aga Khan umemnufaisha Bi Sally kidijitali na kumpa jukwaa la kutalii mbinu tofauti za kufundisha wanafunzi wakiwa nyumbani wakati huu wa janga la corona.