Habari

Kaunti kuanza kupokea fedha wiki hii

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SASA serikali 47 za kaunti zitaanza kupokea mgao wa kwanza wa Sh316.5 bilioni kuanzia wiki hii baada ya fedha hizo kucheleweshwa kwa miezi mitatu.

Hii ni baada ya bunge la kitaifa kupitisha Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARA), 2020 Jumanne jioni ambao sasa unasubiriwa kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta.

Baada ya mswada huo kutiwa saini, Msimamizi wa Bajeti (CoB) ataamuru kusambazwa kwa Sh60 bilioni kwa kaunti, pesa ambazo tayari zimetolewa kutoka Hazina ya Kitaifa.

Sheria hiyo pia itawezesha serikali za kaunti kuanza kupokea Sh13.7 bilioni kutoka kwa serikali kama ruzuku ya miradi maalum; Sh9.4 bilioni za kukarabati barabara na Sh30.2 bilioni kama mikopo ya ruzuku kutoka nje.

Kati ya Sh13.7 bilioni ambazo ni ruzuku kutoka serikali kuu, Sh6.2 bilioni zilitumika kulipia gharama ya ukodishaji vifaa vya kimatibabu chini ya mpango wa MES, Sh4.3 bilioni zitaelekezwa katika hospitali za Level 5, Sh2 bilioni zitaelekezwa kwa vyuo anuwai na Sh300 milioni za kujenga makao makuu ya kaunti.

Wakichangia mijadala kuhusu mswada huo, wabunge waliwashutumu maseneta kwa kuchelewesha mswada huo ambao ni muhimu katika kuwezesha serikali za kaunti kupokea mgao wa fedha zilizotengewa katika bajeti ya kitaifa.

“Inasikitisha kuwa huu ni mwezi wa tatu tangu kuanza kwa mwaka huu wa kifedha Julai Mosi ilhali serikali za kaunti hazijapokea mgao wao wa fedha. Ni kinaya kwamba hali hii imesababishwa na wenzetu katika seneti ambao walivutana kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha hizi kwa kipindi cha miezi mitatu,” akasema kiongozi wa wengi Amos Kimunya.

Naye kiongozi wa wachache John Mbadi alisema kucheleweshwa kwa usambazaji wa fedha kwa kaunti ni kielelezo cha kufeli kwa uongozi katika Seneti.

“Ni jambo la kuhuzunisha kwamba tunazipa kaunti fedha miezi mitatu baada ya kuanza kwa mwaka wa kifedha. Mtu anawezaje kuishi miezi mitatu bila mshahara? Tunaziangusha kaunti zetu. Inasikitisha kuwa wanaofanya hivyo ni maseneta wenye jukumu la kikatiba la kutetea kaunti,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

Wabunge Makali Mulu (Kitui ya Kati), Chris Wamalwa (Kiminini) na mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Kanini Kega walisema sheria inafaa kubadilishwa ili kuwapokonya maseneta wajibu wowote wa kuamua masuala ya ugavi wa fedha kwa kaunti.

Mnamo Jumanne Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya alitisha tena kwamba huenda serikali za kaunti zikalazimika kusitisha shughuli za utoaji huduma kutokana na ukosefu wa fedha.

Nyingi za kaunti zimeshindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi huku zingine, kama Kisumu, zikilazimika kuchukua mkopo kutoka kwa benki ili kuwalipa wafanyakazi wao.