• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Kamworor mkekani AK ikifichua kikosi cha Kenya kwa minajili ya Nusu Marathon ya Dunia nchini Poland

Kamworor mkekani AK ikifichua kikosi cha Kenya kwa minajili ya Nusu Marathon ya Dunia nchini Poland

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limejaza pengo la bingwa mtetezi Geoffrey Kamworor kwenye orodha ya Wakenya watakaoshiriki makala ya 24 ya mbio za Nusu Marathon ya Dunia jijini Gdynia, Poland mnamo Oktoba 17, 2020.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia, Peres Jepchirichir ambaye pia atanogesha kivumbi cha Valencia Half Marathon nchini Uhispania mnamo Disemba 6, 2020, atakuwa sehemu ya watimkaji watakaonogesha mbio hizo za kilomita 21 nchini Poland.

Kuondolewa kwa Kamworor na pengo lake kujazwa, ni miongoni mwa mabadiliko ambayo AK imefanyia kikosi kitakachoshiriki mbio za Nusu Marathon ya Dunia zilizokuwa zifanyike Machi 29, 2020 kabla ya kuahirishwa na kuratibiwa upya kwa sababu ya janga la corona.

Mkurugenzi wa mashindano wa AK, Paul Mutwii amefichua kwamba tayari wameunga kikosi cha wanariadha 10; wanaume watano na wanawake watano watakaopeperusha bendera ya Kenya nchini Poland.

Mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia kwenye marathon, Patrick Makau, atakuwa mwelekezi wa kikosi cha Kenya kwa ushirikiano na bingwa mara mbili wa dunia katika marathon, Catherine ‘The Great’ Ndereba na Patrick Kipsang ambaye ni meneja wa timu.

Wanariadha wa Kenya wamepangiwa kuondoka humu nchini mnamo Oktoba 15, 2020 kuelekea Poland.

Kwa upande wa wanaume, mbio hizo zimemvutia pia Kibiwott Kandie aliyeibuka mshindi wa Ras Al Khaimah (RAK) Half Marathon mnamo Februari 2020. Kandie, aliyeandikisha muda bora wa dunia wa dakika 58:38 jijini Prague, Jamhuri ya Czech mnamo Septemba 6, 2020 atatoana jasho na Leonard Barsoton (59:09).

Shadrack Kimining, aliyeambulia nafasi ya tatu kwenye Houston Half Marathon mnamo Januari ameachwa nje ya kikosi cha Kenya ambacho pia hakitakuwa na Victor Chumo aliyeibuka mshindi wa Guadalajara Half Marathon mnamo Februari, 2020.

Nafasi zao zimechukuliwa sasa na Bernard Kipkorir (59:07), aliyeibuka wa pili kwenye Houston Half Marathon, Houston, USA mnamo Januari 2020 na mshindi wa Prague Half Marathon mnamo 2019, Bernard Kimeli (59:07). Morris Munene (59:22) anakamilisha kikosi hicho cha Kenya kwa upande wa wanaume.

Kamworor, 27, alichelewa kurejea mazoezi baada ya kupata majeraha kadhaa mnamo Juni 25, 2020. Mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia katika nusu marathon, aligongwa na pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi wakati huo na akapata majeraha ya kichwa na kifundo cha mguu. Hata hivyo, alipona baada ya kufanyiwa upasuaji na kutibiwa katika Hospitali ya St Luke’s mjini Eldoret.

Kuachwa nje kwa Kamworor kunamsaza Barsaton aliyeambulia nafasi ya 12 mnamo 2018 kuwa mwanariadha wa pekee aliyepeperusha bendera ya Kenya wakati huo katika kikosi kitakachotegemewa mwaka huu.

Dorcas Jepchumba (1:07:10) aliyeambulia nafasi ya tatu kwenye Prague Half Marathon na Brillian Jepkorir (1:07:12), aliyeridhika na nafasi ya pili kwenye Houston Half Marathon mnamo Februari 2020, wamedumisha nafasi zao kwenye kikosi cha wanawake kinachojumuisha pia Dorcas Jepchirchir na mshindi wa nishani ya fedha katika Nusu Marathon ya Dunia mnamo 2018, Pauline Kaveke.

Mbali na Jepchirchir anayeshikilia rekodi ya dunia ya saa 1:05:34 aliyoiweka kwenye mbio hizo za kilomita 21 wakati wa Prague Half Marathon mnamo Septemba 5, kikosi cha Kenya kina pia mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia Joyciline Jepkosgei (1:04:51).

Mwingine katika kikosi cha Kenya ni Rosemary Wanjiru (1:05:34) aliyeibuka wa tatu kwenye Ras Al Khaimah (RAK) Half Marathon mnamo Februari 2020. Wanjiru, Jepkorir na Jepchumba watakuwa wakiwakilisha Kenya kwa mara ya kwanza.

Jepkosgei aliridhika na medali ya fedha (saa 1:06:54) huku Mwethiopia Netsanet Gudeta akiweka rekodi mpya ya saa 1:06:11 mwaka jana. Hiyo ndiyo rekodi ambayo Jepchirchir aliivuna jijini Prague mwezi mmoja uliopita.

Nusu Marathon za Dunia nchini Poland zimevutia pia Joshua Cheptegei (Uganda) na Sifan Hassan (Uholanzi) ambao ni mabingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000. Hassan atapania kumtoa jasho Mwethiopia Netsanet Gudeta ambaye atalenga kutetea ubingwa wa taji lake.

KIKOSI CHA KENYA:

(Wanaume):

Kibiwott Kandi

Leonard Barsoton

Morris Munene

Bernard Kipkorir

Benard Kimeli

(Wanawake):

Brillian Jepkorir

Dorcas Jepchumba

Peres Jepchirchir

Joyciline Jepkosgei

Rosemary Wanjiru

You can share this post!

Liverpool tuna kibarua kizito – Virgil van Dijk

Harambee Stars ya Kenya kucheza na Chipolopolo ya Zambia...