COVID-19: Kocha wa Ukraine apangwa katika kikosi cha kucheza dhidi ya Ufaransa
Na MASHIRIKA
KOCHA Oleksandr Shovkovskiy wa timu ya taifa ya Ukraine, amejumuishwa katika kikosi kitakachovaana na Ufaransa kwenye mechi ya kupimana nguvu mnamo Oktoba 7, 2020.
Hii ni baada ya kipa chaguo la kwanza Andriy Lunin na Yuriy Pankiv ambaye ni kipa chaguo la pili kutemwa katika kikosi cha Ukraine baada ya kuugua Covid-19.
Shovkovskiy ambaye ni mlinda-lango wa zamani wa klabu ya Dynamo Kiev alistaafu mnamo 2016. Kuugua kwa Lunin na Pankiv kunamsaza Georgiy Bushchan kuwa kipa wa pekee aliye katika hali shwari ya kutegemewa na kocha Andriy Shevchenko kambini mwa Ukraine.
Beki Leo Dubois wa timu ya taifa ya Ufaransa pia hatakuwa sehemu ya mchuano huo utakaochezewa jijini Paris baada ya virusi vya corona kumweka kocha Didier Deschamps katika ulazima wa kumdondosha kikosini.
“Oleksandr Shovkovskiy alitamatisha kipindi chake cha usogora katika timu ya taifa ya Ukraine mnamo Disemba 2016. Licha ya kupokezwa majukumu ya kuwa kocha msaidizi, amekuwa akijituma mazoezini.”
“Ina maana kwamba huenda tukamwajibisha katika mechi dhidi ya Ufaransa iwapo kipa wetu chaguo la tatu, Bushchan pia atapatikana na corona katika dakika za mwisho au atapata jeraha kabla au wakati wa mechi hiyo jijini Paris,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Ukraine.