Wanasoka watatu wa Scotland kukosa mchujo wa Euro baada ya kuugua Covid-19
Na MASHIRIKA
WANASOKA Stuart Armstrong, Kieran Tierney na Ryan Christie wa timu ya taifa ya Scotland watakosa nusu-fainali ya mchujo wa kufuzu kwa fainali za Euro 2021 dhidi ya Israel kwa sababu ya Covid-19.
Japo Armstrong ndiye wa pekee aliyepatikana na virusi vya corona, Tierney ambaye ni beki wa Arsenal na mvamizi Christie wa Celtic watalazimika kujitenga kwa siku 14 zijazo kwa kuwa walitangamana na Armstrong kwa karibu sana kambini.
Watatu hao hawatakuwa pia sehemu ya kikosi cha Scotland kitakachoshiriki mechi za Nations League dhidi ya Slovakia na Jamhuri ya Czech.
Christie atakosa pia mechi itakayowakutanisha Celtic na Rangers mnamo Oktoba 17, 2020 huku Tierney akitarajiwa kukosa gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalowakutanisha na Manchester City siku hiyo hiyo.
Armstrong ambaye ni kiungo wa Southampton, hakupatikana na virusi vya corona alipowasili katika kambi ya Scotland mnamo Oktoba 5, 2020.
Hata hivyo, vipimo vya afya vilivyofanywa na Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) vilibainisha kwamba sogora huyo alikuwa anaugua Covid-19 na hivyo atajitenga kwa siku 10 kuanzia Oktoba 6, 2020.
“Ingawa hizi ni taarifa za kuvunja moyo, muhimu zaidi ni kuzingatia kanuni zilizopo za afya na kuhakikisha kwamba wanakikosi wengine wanasalia katika hali nzuri,” akasema kocha wa Scotland, Steve Clarke.