Makala

NGILA: Teknolojia itumiwe vizuri kudhibiti sekta ya matatu

October 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA wiki za hivi majuzi, maandamano yamekuwa yakishuhudiwa mjini Nakuru, wamiliki wa matatu wakipinga agizo la serikali ya kaunti hiyo kuwafurusha kutoka katikati ya jiji ili kupunguza msongamano.

Ingawa ni wazo zuri kupunguza msongamano unaochangia pakubwa wizi wa simu katika miji mingi hapa Kenya, kwa kawaida serikali ya Kaunti ya Nakuru haijajenga steji za hadhi nje ya mji, hali inayosababisha kukithiri kwa makabiliano baina ya polisi na wenye matatu.

Lakini hiyo si taswria kamili. Tukirudi nyuma miaka sita iliyopita, serikali ya kitaifa ilikuwa imependekeza mpango thabiti wa kupunguza masongamano kwa kutumia teknolojia.

Kwa kujibu swali la ni nini kiini cha misongamano, serikali ilikuwa imebaini ni mwenendo wa baadhi ya madereva wakora kutoka kuwavuka wenzao kwenye orodha ya kupakia abiria kwa kutumia njia za mikato ili mwisho wa siku wapate hela nyingi.

Ili kuzima tabia hiyo, serikali ilikuwa imebuni sera madhubuti kupitia Wizara ya Uchukuzi kuondoa vikwazo katika biashara hiyo kwa kutumia teknolojia ya malipo ya kidijitali.

Kanuni hizo zilishapishwa kwenye ilani ya kisheria chini ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) mnamo September 2013.

Sheria hiyo ilinuia pia kuondoa wakora kwenye sekta ya matatu, kulainisha malipo, kuzima ufisadi na mtindo wa kuwahonga maafisa wa trafiki kupitia mfumo wa dijitali ambao ungfuatilia kila gari na malipo ya kila abiria, kila siku.

Zikiwania zaidi ya Sh200 bilioni katika sekta hiyo, kampuni za Google, Safaricom, Equity Bank, Mastercard, KCB na benki ya Family zilijitokeza mara moja kusaidia kutoa suluhu kwa changamoto hizo.

Miradi ya malipo ya kidijitali kama vile Bebapay, Mastercard Fare Card, Pesa Mob na 1963 Card ilianzishwa kuteka mabilioni ya hela za nauli kutoka kwa abiria.

Lakini miaka saba baadaye, Kenya bado imo kandi lindi lile lile la 2013 ambapo wamiliki wa matatu, benki na kampuni za kiteknolojia hazijakubaliana kuhusu suluhu hiyo licha ya kutumia mamilioni.

Mojawapo ya changamoto ni kuwa baadhi ya mafisadi ambao wanafaidi pakubwa kutokana na uchukuzi walihujumu jitihada hizo, kwa kuagiza vifaa vya malipo ya kidijitali kutoka China vyenye kasoro na visivyoweza kudumisha chaji ya betri kwa muda mrefu.

Uchunguzi wangu umeonyesha kuwa licha ya wafadhili kuagiza maelfu ya vifaa hivyo ili kila matatu iwe na chake, vilifeli vilipofika Nairobi kwani berti zake hazingesitiri shughuli nzima ya kupisha nauli na kufuatilia kila gari kwenye laini kwa zaidi ya saa tatu.

Ikawa na mzaha mchafu wa kuhakikisha suluhu hizo hazitazaa matunda. Taswria ikajichora ya serikali isiyoweza kuthibiti sekta muhimu, maafisa wasioweza kukubali ufisadi kutokomezwa.

Lakini bado kuna matumaini. Serikali kupitia NTSA inafaa kuandaa midahalo kuwahusisha wamiliki wa matatu, madereva, wafadhili na kampuni za teknolojia na kukubaliana ni asilimia ngapi ya hela zinaundwa na kila gari inafaa kumwendea kila mshikadau.