AKILIMALI: Kwake kondoo ni nyama na sufu
Na RICHARD MAOSI
NYANDA za juu zenye baridi kali katika eneo la Bonde la Ufa ni mojawapo ya maeneo mwafaka kufuga kondoo kwa ajili ya nyama na manyoya yake (sufu).
Kondoo ni wanyama wanaoweza kufugwa kwa gharama nafuu kutokana na uwezo wao mkubwa wa kukabiliana na aina mbalimbali ya changamoto zinazoweza kuwakumba kama vile uhaba wa malisho.
Katika mazungumzo ya kipekee na Akilimali, Bw Erick Kiprotich Kirior kutoka eneo la Mlango kaunti ya Nandi anasema alianza kufuga kondoo mwaka wa 2007 ili kujiongezea kipato baada ya kustaafu kazi ya uhandisi.
Alilenga kujiajiri na kuwaajiri vijana kutoka eneo la Nandi, sehemu ambayo ina utajiri mkubwa katika sekta ya kilimo na ufugaji.
“Mimi hufuga mchanganyiko wa kondoo aina ya kienyeji na wale wa merino, bridi ambazo zinaweza kustahimili mazingira magumu iwe ni baridi au jua kali,”akasema.
Anasema kwa sababu wafugaji wengi huazimia kuwafuga kondoo kwa ajili ya nyama tu, Kiprotich alilenga kufaidika kwa sufu pamoja na kuwauza wakati wa misimu ya sherehe kama vile krismasi na kila mwisho wa mwaka.
Anasema wanunuzi wake wengi ni wamiliki wa mikahawa kutoka kaunti jirani ya Uasin Gishu, wafugaji wa kibinafsi, wamiliki wa vichinjio na taasisi za kufanya utafiti kama vile KARLO, miongoni mwa nyingine.
Kwa kawaida bei ya kondoo wa kike ni baina ya Sh8,000-12,000 huku kondoo dume akiuzwa kati ya Sh13,000 hadi-15,000. Hata hivyo, wakati wa shamrashamra za sherehe mwisho wa mwaka bei ya kondoo inaweza kupanda mpaka Sh18,000 kwa jinsia zote.
Kiprotich anaongeza kuwa katika mazingira ya kufugia kondoo, kibanda cha kondoo kinahitaji kuwa katika sehemu ambayo ni salama wasije wakashambuliwa na wanyama kama mbwa koko. Aidha, sehemu hiyo isiwe ya kufanya maji kutuama, hususan wakati wa mvua nyingi, kwani katika kipindi hiki mkurupuko wa maradhi hutokea na kumgharimu mkulima hela nyingi wakati wa kuwatibu.
“Hii ina maana kuwa ni lazima mkulima atie juhudi nyingi na jasho katika kuhakikisha kondoo wake wana afya na kufuatilia historia ya viumbe hawa kwa kuhifadhi kumbukumbu zake,”asema.
Kiprotich anasema kuwa msimu wa baridi shadidi ni baina ya Aprill na Julai na wakati huo malisho huwa yanapatikana kwa wingi mashambani.
“Hata hivyo msimu wa kiangazi sisi huwalisha kondoo kwa majani ya kawaida tu. Wakati mwingine tunawapimia lishe wasije wakazoea kula chakula kwa wingi,”alisema.
Lishe ambayo ni mchanganyiko wa viazi vitamu, mboga za sukumawiki au kabeji, husaidia kondoo kunenepa baada ya muda mfupi na kuwavutia wanunuzi.
Yeye hulisha kondoo wake wenye umri wa mwaka mmoja na zaidi kwa mboga anazokuza katika shamba lake mbali na kuongezea lishe za ziada, ambazo ni mabaki ya mahindi yaliyosagwa na kuchanganywa na sukari nguru.
Kondoo waliokomaa hujisakia michicha inayokuwa pembeni ya shamba lake akisema wanyama hawa wana tabia ya kuchagua sana majani na ndiyo sababu si rahisi wapate maradhi. Kiprotich anasema kwamba kufuga kondoo ni kazi anayojivunia. Ni aina ya kilimo ambacho wakati mwingine yeye hulazimika kukata manyoya mara moja kila mwaka na kuuza kwenye viwanda vinavyotengeneza nguo na blanketi.
“Mimi huwaajiri watalamu wa kukata manyoya kulingana na idadi ya kondoo wanaokatwa manyoya kila siku,” asema huku akiongeza kuwa inategemea ni aina ngapi ya kondoo wanaoshughulikiwa.
Kilomita 150 kutoka kaunti ya Nandi tunakutana na Mzee Maurice Mugo katika barabara ya Olkalou-ukielekea kaunti ya Nyandarua.
Akiwa mmiliki wa shule, yeye hutumia tija inayotokana na ufugaji wa kondoo kuwalipa walimu wake mshahara wakati huu wa janga la covid-19, tangu Machi wizara ya elimu ilipofunga shule.
Kwa mujibu wa Mugo, anawafuga kondoo kwa sababu wao humsaidia kupata mbolea ambayo yeye hutumia kukuza mboga kwani yeye pia ni mkulima wa nyanya, vitunguu na spinach.
Pili, anasema kuwa aliamua kuwafuga kondoo kwa sababu hawana gharama kubwa na kwamba mkulima hahitaji idadi kubwa ya wafanyakazi kuwaangalia.
“Isitoshe kondoo huzaana mara kwa mara na watoto wao huchukua muda wa miezi minane hivi kukomaa,”asema.
Kwa mujibu wa mzee Mugo, yeye anawafuga kondoo aina ya Bellary na Merino ambapo yeye huwalisha kwa mchanganyiko wa mahindi yaliyosagwa vyema na kuchanganywa na madini ya calcium au phosphorus.
Kufikia sasa anamiliki zaidi ya kondoo 100. Wateja wake wengi ni wafugaji na wafanyabiashara kutoka kaunti ya Nyahururu, Molo, Uasin-Gishu, Nairobi na Nyeri.