Raila asema ODM tayari kuonyesha wapinzani kivumbi Msambweni
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amewaambia wapinzani wa chama hicho katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha ubunge cha Msambweni kuwa tayari kwa mapambano makali.
Huku akionekana kumrejelea Naibu Rais William Ruto ambaye anampigia debe mgombea wa kujitegemea katika uchaguzi huo mdogo Feisal Abdalla Bader, Bw Odinga amewaonya dhidi ya kutumia uchaguzi huo kama jukwaa la kuchapa siasa za urais za mwaka 2022.
“Sisi tunaenda Msambweni kuwapa wafuasi wetu kiongozi atakayekamilisha miradi ya maendeleo ambayo marehemu Suleiman Dori alianzisha. Lakini mtu fulani anaenda huku kutafuta kura ya urais. Tunataka kumwambia kwamba tutamwonyesha cha mtema kuni,” akasema Jumatano katika makao makuu ya ODM, Nairobi.
Hii ni baada ya kuongoza hafla ya kumkabidhi rasmi tiketi mgombea wa ODM katika uchaguzi huo mdogo Omar Boga.
Wengine waliokabidhiwa rasmi vyeti vya uteuzi ni wapeperusha bendera ya ODM katika chaguzi ndogo za udiwani; Samuel Dede (wadi ya Kisumu Kaskazini) na Jimmy Mwamibi wa wadi ya Wundanyi/Mbale.
Kwa mara nyingine alikosoa mpango wa Naibu Rais wa kuwapa vijana na akina mama vifaa mbalimbali vya kujisaidia kuchuma mapato akisema hiyo inaonyesha wazi kuwa Dkt Ruto amefeli katika ajenda yake ya kuzalisha nafasi 500,000 za kazi kila mwaka.
“Mnamo 2013 uliwaahidi vijana nafasi 500,000 za ajira kila mwaka lakini baada ya miaka saba hizo nafasi za kazi haziko. Sasa unawahadaa kwa kuwapa wilbaro na mikokoteni. Sisi tunaamini kuwa suluhu ni kuwafunza watu wetu mbinu za kiubunifu za kuwawezesha kuzalisha mali,” akasema Bw Odinga.
Kwa upande wake Bw Boga alielezea imani kwamba ataibuka mshindi katika uchaguzi huo mdogo utakaofanyika mnamo Desemba 15, 2020.
“Naambia wafuasi wa ‘Tangatanga’ kwamba tuko tayari kuwakabili. Tutawashinda pamoja na vikaragosi wao kule Msambweni,” akaeleza.
Alisema hayo huku duru zikisema kuwa Dkt Ruto anajaribu kuwashawishi wagombeaji wengine wajiondoe na wamuunge mkono Bw Bader.
Maseneta wa zamani Johnstone Muthama, Hassan Omar na Boni Khalwale ndio wataongoza kampeni za kumpigia debe mgombea huyo ambaye alihudumu kama msaidizi wa marehemu Dori.
Naye Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho anatarajiwa kuongoza kampeni ya kumpigia debe mgombea wa ODM.