• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Ujerumani wala sare ya tatu mfululizo chini ya kocha Joachim Loew

Ujerumani wala sare ya tatu mfululizo chini ya kocha Joachim Loew

Na MASHIRIKA

UTURUKI walifunga bao la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwalazimishia mabingwa wa dunia wa 2014 sare ya 3-3 katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha jijini Cologne mnamo Oktoba 7, 2020.

Uturuki walitoka nyuma mara tatu kupitia kwa mabao ya wachezaji Ozan Tufan, Efecan Karaca na Kenan Karaman.

Ujerumani walijipata uongozini mara tatu kupitia kwa mabao ya Julian Draxler, Florian Neuhaus na Gian-Luca Waldschmidt ambayo yalichangiwa na sajili mpya wa Chelsea, Kai Havertz.

Ujerumani waliokuwa chini ya unahodha wa Draxler, walikosa idadi kubwa ya wanasoka wao tegemeo katika mechi hiyo iliyowashuhudia wakipoteza nafasi nyingi za wazi.

Kocha Joachim Loew wa Ujerumani aliwaacha nje wachezaji Manuel Neuer na Serge Gnabry wa Bayern Munich ambao atapania kuwategemea pakubwa kwenye mechi zijazo za Uefa Nations League.

Ujerumani wamepangiwa kuvaana na Ukraine ugenini mnamo Oktoba 10, 2020 kabla ya kuwa wenyeji wa Uswisi katika gozi jingine la Nations League mnamo Oktoba 13, 2020.

Hofu zaidi kwa mashabiki wa Ujerumani ni kwamba hawajawahi kusajili ushindi katika mchuano wowote tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020. Hadi walipokutana na Uturuki, Ujerumani walikuwa wamelazimishiwa sare mbili nyinginezo katika mechi mbili za Nations League kwenye Kundi A4 dhidi ya Uhispania na Uswisi.

Mbali na Havertz, wachezaji wengine walioridhisha pakubwa kwa upande wa Ujerumani katika mechi iliyowakutanisha na Uturuki ni beki wa Chelsea, Antonio Rudiger na kipa wa Arsenal, Bernd Leno.

Kupumzishwa kwa Neuer kulimpa Leno fursa ya kuchezeshwa na timu ya taifa ya Ujerumani kwa mara ya nane.

Ingawa mashabiki 9,200 walitarajiwa kuhudhuria mchuano huo, ni 300 pekee ndio walioruhusiwa kuingia uwanjani Rhein Energie.

You can share this post!

Kibiwott Kandie amtumia salamu Joshua Cheptegei

Vifo kutokana na corona vyagonga 100,000 India