• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Scotland sasa pua na mdomo kufuzu kwa fainali za Euro kwa mara ya kwanza baada ya miaka 23

Scotland sasa pua na mdomo kufuzu kwa fainali za Euro kwa mara ya kwanza baada ya miaka 23

Na MASHIRIKA

SCOTLAND wamesalia na mchuano mmoja pekee kabla ya kufuzu kwa kivumbi cha Euro 2021 – fainali za haiba kubwa zaidi watakazoshiriki katika ulingo wa soka kwa mara ya kwanza tangu 1998.

Hii ni baada ya kikosi hicho kuwapokeza Israel kichapo cha 5-3 kupitia penalti kwenye mchujo uliowakutanisha Oktoba 8, 2020.

Kenny McLean aliwafungia Scotland penalti ya ushindi na kuwakatia tiketi ya kuvaana sasa na Serbia ya kocha Steve Clarke mnamo Novemba 12, 2020.

Mchujo kati ya Scotland na Israel ulichezewa ndani ya uwanja mtupu. Licha ya kukosa huduma za wanasoka kadhaa mahiri, Scotland walitumia vyema uwanja wao wa nyumbani na kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya mechi sita zilizopita.

Kwa upande wao, Serbia walijikatia tiketi ya kuvaana na Scotland baada ya kuwapepeta Norway 2-1 jijini Oslo.

Stuart Armstrong, Kieran Tierney, Ryan Christie, Scott McKenna, Liam Palmer, James Forrest na Oliver Burke ni miongoni mwa wanasoka waliokosa mechi hiyo kwa upande wa Scotland waliotegemea pakubwa maarifa ya Oli McBurnie na Lyndon Dykes kwenye safu ya mbele.

Armstrong, Tierney na Christie walitupwa nje ya kikosi kilichotegemewa na Scotland kwenye nusu-fainali ya mchujo huo dhidi ya Israel kwa sababu ya Covid-19.

Japo Armstrong ndiye wa pekee aliyepatikana na virusi vya corona huku Tierney ambaye ni beki wa Arsenal na mvamizi Christie wa Celtic wakilazimika kujitenga kwa siku 14 zijazo kwa kuwa walitangamana na Armstrong kwa karibu sana kambini.

Watatu hao hawatakuwa pia sehemu ya kikosi cha Scotland kitakachoshiriki mechi zijazo za Nations League dhidi ya Slovakia na Jamhuri ya Czech.

Christie atakosa pia mechi itakayowakutanisha Celtic na Rangers mnamo Oktoba 17, 2020 huku Tierney akitarajiwa kukosa gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalowakutanisha na Manchester City siku hiyo hiyo.

Mechi dhidi ya Israel ilikuwa ya kwanza kati ya 55 kushuhudia Scotland wakikosa kufunga bao tangu Novemba 2013 dhidi ya Amerika.

Scotland kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote kati ya sita zilizopita. Walishindwa mara ya mwisho mnamo Oktoba 2017 chini ya kocha Gordon Strachan.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Scotland kukamilisha mechi bila kuelekeza shuti lililolenga shabaha langoni pa wapinzani tangu walipovaana na Ubelgiji mnamo Septemba 2013.

Scotland kwa sasa watakuwa wenyeji wa Slovakia mnamo Oktoba 11, 2020 kwa minajili ya mechi ya Uefa Nations League uwanjani Hampden.

You can share this post!

Korti yaruhusu LSK kuandamana kuhusu Bunge

RIZIKI: Kozi za mikono na kiufundi ni muhimu kukabili...