Kipa Mendy arejea Chelsea baada ya kupata jeraha kabla ya mechi ya kirafiki kati ya Senegal na Morocco
Na MASHIRIKA
KIPA Edouard Mendy amerejea kambini mwa Chelsea kuendelea na matibabu baada ya kupata jeraha la paja akishiriki mazoezi na timu yake ya taifa ya Senegal.
Mendy, 28, aliingia katika sajili rasmi ya Chelsea kwa mkataba wa miaka mitano mwishoni mwa Septemba 2020 na hakufungwa bao katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha waajiri wake na Crystal Palace mnamo Oktoba 3, 2020.
Chelsea walisajili ushindi wa 4-0 katika mchuano huo ugani Stamford Bridge.
Mendy alirejea jijini London usiku wa Oktoba 8, 2020 baada ya madaktari waliokuwa wakimshughulikia katika hospitali moja jijini Rabat, Morocco kutathmini ukubwa wa kiwango cha jeraha lake.
Senegal wamepangiwa kuvaana na Morocco kirafiki jijini Rabat mnamo Oktoba 9, 2020.
Chelsea walimsajili Mendy kutoka Rennes ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitano ilia toe ushindani mkali kwa kipa wao wa sasa chaguo la kwanza, Kepa Arrizabalaga.
Hadi alipotua ugani Stamford Bridge, mlinda-lango huyo alikuwa amewajibishwa mara 25 na Rennes katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) tangu aingie katika sajili rasmi ya kikosi hicho baada ya kuagana na Reims ya Ufaransa mnamo 2019.
Msimu uliopita wa 2019-20, Mendy hakufungwa katika mechi tisa kati ya 24 za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ikilinganishwa na rekodi ya Kepa ambaye hakufungwa bao katika mechi nane pekee kati ya 33 za EPL.
Ina maana kwamba Mendy aliokoa asilimia 76.3 ya mabao na akafungwa goli kila baada ya dakika 114. Kwa upande wake, Kepa aliokoa asilimia 53.5 ya mabao huku akifungwa goli kila baada ya dakika 63. Hata hivyo, Kepa alikamilisha asilimia 79.7 ya pasi ikilinganishwa na asilimia 70.1 ya Mendy.
Mendy amechezea timu ya taifa ya Senegal mara nane na alikuwa mwanasoka wa nane kusajiliwa na Chelsea katika muhula wa uhamisho wa wachezaji uliokamilika Oktoba 5, 2020.
Kwa kuingia Chelsea, alifuata nyayo za kipa wa zamani wa kikosi hicho, Petr Cech aliyetua ugani Stamford Bridge kutoka Rennes mnamo 2004. Cech ambaye pia amewahi kudakia Arsenal, sasa ni mkurugenzi wa kiufundi kambini mwa Chelsea na mshauri wa makipa.