Mashirika ya kijamii yasema ni vizuri masharti ya NSAC yasihujumu uhuru na haki za kimsingi
Na CHARLES WASONGA
BAADHI ya Mashirika ya Kijamii nchini yametaka masharti yaliyotolewa na Baraza la Ushauri kuhusu Usalama (NSAC) yakilenga kudhibiti wanasiasa, vyombo vya habari na umma kwa jumla, yasitumike kuhujumu uhuru na haki za kimsingi za binadamu.
NSAC ilisema inalenga kuzima usambazaji wa matamshi ya chuki yanayoweza kuchochea fujo na uhasama nchini.
Huku baadhi ya mashirika hayo yakisema masharti yaliyotolewa Jumatano na mwenyekiti wa baraza hilo Joseph Kinyua, sio mageni, wengine wanasema masharti hayo yanaweza yakatumiwa kuhujumu haki za kimsingi za Wakenya.
Shirika la Amnesty International limewataka maafisa wa serikali, polisi wakiwemo, kuzingatia hitaji la vipengee vya 21 na 245 vya Katiba vinavyowahitaji kutojiingiza katika siasa na kuendesha majukumu yao bila mapendeleo.
Kwenye taarifa, Mkurugenzi Mkuu wake Irungu Houghton amesema polisi hawafai kukubali kutumika kuhujumu haki ya raia ya kujumuika, kutoa maoni na haki zao za kisiasa.
“Katika utekelezaji wa kanuni hizi zilizotolewa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua, polisi wasionekane kuingilia au kuhujumu haki za Wakenya kutangamana na kuvumisha sera za kisiasa wanazotaka,” akasema.
Bw Irungu ameongeza kuwa kipengele cha 37 cha Katiba kinasema kuwa kila mtu ana uhuru kujumuika na kushiriki maandamano ya amani.
“Kile waandalizi wa mikutano hiyo wanapaswa kufanya ni kuwaarifu maafisa wa usalama ili wapewe ulinzi,” anaeleza.
Bw Irungu ameongeza kuwa kipengele cha 34 cha Katiba kinazuia serikali kuadhibu mtu yeyote kwa misingi ya kutoa maoni kupitia chombo chochote cha habari.
Vipengele vya 33 na 35, akaongeza, pia vinalinda uhuru wa vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Malalamishi yote dhidi ya vyombo vya habari, inafaa yawasilishwe kwa Baraza la Vyombo vya Habari (MCK), ambalo lina jopo maalum la kusikiza na kuamua malalamishi hayo,” akasema.
Naye mkurugenzi mkuu wa Shirika la International Centre for Policy & Conflict (ICPC) Ndung’u Wainaina amesema baraza la NSAC lilikosea kwa kutoa masharti hayo.
Amesema Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) ndilo lenye mamlaka ya kikatiba kutoa masharti kama hayo.
“Kinyua na kundi lake sio watu wanaoruhusiwa kisheria kutoa taarifa kama hiyo. Taarifa na masharti hayo kwa pamoja vilifaa kutolewa na baraza la kitaifa la usalama linaloongozwa na Rais,” Bw Wainaina akaeleza.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Bw Kinyua, ambaye pia ndiye Mkuu wa Utumishi wa Umma, alihujumu uhuru wa vyombo vya habari kupitia masharti aliyotoa.
“Vile vile, kundi hilo lilidhibiti haki na uhuru wa Wakenya kujumuika. Mahakama zimeamuru kila wakati kwamba watu hawawezi kunyimwa haki ya kujumuika au kutangamana,” akasema Bw Wainaina ambaye ni wakili.
Kwa upande wake Mshirikishi Mkuu wa Muungano wa Mashirika ya Kijamii Nchini Suba Churchil anasema Kinyua na wenzake hawakutangaza chochote kipya, ila alinukuu sehemu ya 5 ya sheria inayodhibiti mikutano ya hadhara.
“Kwa hivyo, baadhi ya Wakenya walifasiri taarifa aliyotoa Bw Kinyua kama ambayo ililenga kudhibiti kundi fulani la watu. Hii ni kwa sababu ilitolewa siku tatu baada ya fujo zilizoshuhudiwa mjini Kenol, Kaunti ya Murang’a saa chache kabla ya Naibu Rais William Ruto kuhudhuria ibada ya Jumapili na hafla ya harambee,” akasema Bw Suba.
Akaongeza: “Hata siku tatu ambazo alisema waandalizi wa mikutano ya hadhara wanapasa kuwajulisha wakuu wa polisi katika eneo husika sio geni kwa sababu tayari ipo katika sheria.”
Kulingana na Bw Kinyua, mtu yeyote anayepanga kuandaa mkutano wa hadhara anapaswa kumjulisha Afisa Mkuu wa Polisi, siku tatu kabla wala sio kabla ya siku 14 kama ilivyokuwa zamani.
Na vyombo vya habari vimepigwa marufuku kupeperusha matamshi ya chuki yatakayotolewa na wanenaji katika mikutano kama hiyo.
Amri kama hiyo pia imetolewa kwa mitandao ya kijamii na wasimamizi wayo.