Michezo

De Bruyne kutia saini mkataba mpya utakaomvunia Sh42 milioni kwa wiki kambini mwa Manchester City

October 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KIUNGO Kevin De Bruyne, 29, anatarajiwa wiki hii kutia saini mkataba wa miaka miwili utakaomshuhudia akipokezwa mshahara wa Sh42 milioni kwa wiki kambini mwa Manchester City.

Kwa sasa, nyota huyo raia wa Ubelgiji anatia mfukoni kima cha Sh39 milioni kwa wiki ugani Etihad, na kandarasi yake inatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa 2023.

De Bruyne ambaye pia amewahi kuchezea Chelsea ya Uingereza na Wolfsburg nchini Ujerumani, tayari amehudumu ugani Etihad kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Katika mahojiano yake na gazeti la AS nchini Uhispania mnamo Juni, De Bruyne alikiri kuwa anayafurahia maisha yake uwanjani Etihad ila angekuwa radhi kukabiliana na changamoto mpya kwingineko iwapo marufuku yaliyokuwa yazuie Man-City kushiriki kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa miaka miwili yangedumishwa.

Mwezi mmoja kabla ya mahojiano hayo, De Bruyne alikuwa ameliambia gazeti la HLN nchini Uingereza kwamba angehiari kuyoyomea Barcelona au Real iwapo Man-City wangesalia nje ya kivumbi cha UEFA kwa misimu miwili mfululizo.

Tangu ajiunge na Man-City baada ya kushawishiwa kuagana na Wolfsburg kwa kima cha Sh7.5 bilioni mnamo Agosti 2015, De Bruyne amekuwa kipenzi cha mashabiki wengi katika soka ya Uingereza jijini Manchester na amesaidia Man-City kutia kapuni jumla ya mataji saba ya haiba kubwa.

Wakati uo huo, kocha Pep Guardiola amesema kwamba kupona kwa beki wa kushoto, Joao Cancelo ni afueni kubwa kwa Man-City ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Arsenal ligini.

Cancelo ambaye ni raia wa Ureno, hajachezeshwa na Man-City katika jumla ya mechi tano zilizopita kutokana na jeraha la mguu.

Jeraha la muda mrefu ambalo limekuwa likiuguzwa na Cancelo pamoja na kusuasua kwa kiungo raia wa Ukraine, Oleksandr Zinchenko ni miongoni mwa sababu zilizomchochea kocha Guardiola kuanza kuyahemea maarifa ya nyota Nicolas Tagliafico wa Ukraine pamoja na David Alaba wa Bayern Munich.

Wakati akiwa nje kwa jeraha, nafasi ya Cancelo kambini mwa Man-City imekuwa ikijazwa ama na Benjamin Mendy au Zinchenko.

Cancelo alisajiliwa na Man-City kutoka Juventus kwa Sh8.4 bilioni mnamo 2019. Anakuwa miongoni mwa wanasoka wa hivi karibuni kurejea kambini mwa Man-City baada ya fowadi Sergio Aguero na kiungo Ilkay Gundogan.