Makala

Ruiru, mtaa unaokua kwa kasi kufuatia kujengwa kwa Thika Superhighway

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KATIKA barabara ya Thika Road maarufu kama Thika Superhighway, pembezoni ni mitaa kadhaa.

Kati ya Juja na Githurai, ni mtaa wa Ruiru ambao ramani inasoma upo katika Kaunti ya Kiambu.

Mtaa wa Ruiru ni wenye shughuli chungu nzima, kuanzia biashara, uchukuzi, uwekezaji wa majengo ya kukodi na kupangisha.

Tangu kuzinduliwa kwa Thika Road, ambayo ni barabara kuu nchini, mtaa huo umekua kwa kasi.

Ni mtaa wenye viwanda kadhaa, kama vile cha mabati ya ujenzi na kuezeka nyumba, magodoro na vingine vya kutengeneza mbolea, kati ya vinginevyo.

Richard Ngunjiri ni mmiliki wa kiwanda cha uundaji wa mboleahai, kinachofahamika kama Organic Fields na anasema kuimarishwa kwa miundomsingi Ruiru kumechangia eneo hilo kustawi.

“Thika Superhighway imechangia kuimarika kwa eneo la Ruiru. Kiwanda changu cha utengenezaji wa mboleahai kuimarisha mazao ya kilimo kinajivunia kuimarika kwa miundomsingi Ruiru,” Ngunjiri anasema.

Ni katika viunga vya mtaa huo, hususan maeneo yenye mashamba, ambapo shughuli za kilimo na ufugaji zimenoga.

Pioneer Farm Feeds ni miongoni mwa kampuni zinatoa huduma kwa wafugaji. Aidha, kampuni hiyo iliyoko Mjini Ruiru hutengeneza na kuuzia wakulima na wafugaji chakula cha kuku.

Miundomsingi bora Ruiru ilivyochangia kuimarika kwa eneo hilo. Picha/ Sammy Waweru

Ilianzishwa mwaka wa 1995, na pia huangua vifaranga wa kienyeji walioimarishwa.

“Thika Road ilipoimarishwa, biashara zimeendelea kunoga. Ruiru inakua kwa kasi na Pioneer Farm Feeds inahisi mabadiliko, nikilinganisha na miaka ya awali,” anaeleza James Mburu, meneja mkuu wa kampuni hiyo.

Thika Superhighway ilijengwa kati ya 2009 na 2012, chini ya utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, mradi uliogharimu kiasi cha Sh32 bilioni.

Ni katika mtaa uo huo wa Ruiru, bucha zimesheheni, na ambazo hualika mamia na maelfu ya watu kununua nyama choma.

Kamakis, kati ya Ruiru Bypass na Ruai, katika barabara inayounganisha Thika Road na Embakasi, ni eneo tajika kwa nyama choma na vinywaji.

Mchana na mwendo wa jioni, Kamakis huwa egesho la magari ya hadhi tofauti, kilele kikiwa wikendi ambapo biashara ya nyama na vinywaji hushika kasi.

Kutokana na maendeleo hayo, bei ya ploti Ruiru haikamatiki na vipande vya ardhi vinavyopatikana vikiwa mithili ya mahamri moto sokoni, wengi wakizitaja kuwa ‘hot cake’.

Isitoshe, Ruiru ina shule, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ishara kuwa sekta ya elimu humo imeboreka. Makazi na nyumba za kupangisha za bei nafuu si hoja, maendeleo ambayo yanachangia kusitiri wenye mapato ya chini, kadri na ya juu.