Michezo

Ujerumani walaza Ukraine na kuvuna ushindi wa kwanza katika kivumbi cha Uefa Nations League

October 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

UJERUMANI walisajili ushindi wao wa kwanza katika kipute cha Uefa Nations League kwa kupepeta Ukraine 2-1 katika mchuano uliohudhuriwa na takriban mashabiki 20,000 uwanjani Kyiv Olympic mnamo Oktoba 10, 2020.

Hadi waliposhuka dimbani kuvaana na Ukraine, Ujerumani ambao wanatiwa makali na kocha Joachim Loew, hawakuwa wameshinda mechi yoyote ya Nations League kati ya sita za awali.

Ujerumani walifungua ukurasa wao wa mabao katika dakika ya 20 kupitia kwa Matthias Ginter kabla ya kiungo mvamizi wa Bayern Munich, Leon Goretzka kuchuma nafuu kutokana na masihara ya kipa Georgiy Bushman na kufunga goli la pili katika dakika ya 49.

Penalti iliyofungwa na Ukraine kupitia kwa Ruslan Malinovskyi katika dakika ya 76 ilizidisha ushindani katika mechi hiyo iliyokamilika kwa hisia kali.

Ujerumani ambao hawakushinda mechi yoyote katika makala ya kwanza ya Nations League miaka miwili iliyopita, sasa wanajivunia alama tano kutokana na mechia tatu za hadi kufikia sasa katika kampeni za kivumbi hicho muhula huu wa 2020-21.

Mashabiki walikubaliwa kuhudhuria mchuano huo baada ya maafisa wa afya kutoa idhini ya mahudhurio ya hadi asilimia 30 pekee kwenye uwanja huo wa Kyiv Olympic ulio na uwezo wa kubeba jumla ya mashabiki 70,000.

Beki Antonio Rudiger ambaye hajawajibishwa na Chelsea katika mchuano wowote hadi sasa msimu huu, aliridhisha sana kwa upande wa Ujerumani, akawahaingaisha mabeki wa Ukraine na akachangia bao la kwanza lililofungwa na timu yake ya taifa.

Wachezaji wenza wa Rudiger kambini mwa Chelsea, Kai Havertz na Timo Werner walianza mechi hiyo kwenye benchi ya timu ya taifa ya Ujerumani waliotawazwa mabingwa wa dunia mnamo 2014 fainali za Kombe la Dunia zilipoandaliwa nchini Brazil.

Havertz na Werner waliingia ugani katika kipindi cha pili ili kusaidia Ujerumani kuhimili presha kutoka kwa Ukraine waliokuwa wakiwania fursa ya kusawazisha.